Friday, 28 December 2018

KAULI YA SUMAYE,ZITTO KABWE BAADA YA TUNDU LISSU KUSEMA ATAGOMBEA URAIS 2020

...
Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamesema wanamsubiri kwa hamu Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu apitishwe na chama chake kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Lissu anayetibiwa nchini Ubelgiji baada ya shambulio la risasi zaidi ya 30 lililotokea Septemba 7, mwaka jana akiwa Dodoma, juzi aliliambia gazeti la Mwananchi kwamba hatakuwa na kipingamizi ikiwa chama chake kitampitisha kuwania nafasi hiyo.


Kauli ya Lissu ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya CCM, imepokewa kwa furaha na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakiamini anaweza kutoa ushindani mkubwa kwa mgombea wa chama tawala.


Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe alisema Lissu atavifaa vyama hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Maoni ya Rungwe yaliungwa mkono na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alisema hana shida na kauli ya Lissu.


“Jambo la muhimu kuliko yote ni kuwa mwaka 2019, kwetu ni mwaka wa kudai demokrasia. Azimio la Zanzibar limeweka mpango maalumu wa kukabiliana na ukandamizaji wa demokrasia. Tundu Lissu ni kiongozi muhimu katika harakati hizo,” alisema Zitto.

Pia, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema Lissu hajafanya kosa kutoa kauli hiyo kwa sababu mwanachama yeyote anaweza kueleza nia yake.


“Sijamsikia, lakini kama atapitishwa na chama sioni tatizo, kwa sababu kila chama kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea na ni lazima ufuatwe,” alisema Sumaye.


Sumaye ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa chama hicho alisema Lissu si wa kwanza, “Nimemsikia hata mheshimiwa (Edward) Lowassa, mimi sioni tatizo kama mtu anafuata utaratibu wa chama.”


Chanzo - Mwananchi
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger