Katika kuhakikisha kwamba mnunuzi wa bidhaa hapunjwi, Wakala wa Vipimo Nchini (WMA), wameendelea kufanya ukaguzi wa mizani zinazotumika sehemu tofauti hasa kwa wauzaji wa zao la korosho.
Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kubaini mizani zisizo na viwango ambazo hazitoi kipimo kinachostahili.
WMA ilitembelea baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika ili kushuhudia hali halisi ya upimaji korosho za wakulima.
Meneja wa WMA, mkoa wa Pwani, Evarist Masengo, alisema katika kuhakikisha wakulima wanauza mazao yao kwa kutumia mizani sahihi iliyohakikiwa na wakala huo, mizani 109 zimehakikiwa na kupigwa chapa ya Serikali.
Alisema mkoa wa Pwani una jumla ya vyama vya msingi (AMCOS) 95, ambavyo vinapatikana katika wilaya saba.
Wilaya na idadi ya vyama kwenye mabano ni Mkuranga (39), Kibaha (8), Bagamoyo (3), Chalinze (3), Kisarawe (2), Mafia (1), Rufi ji (13) na Kibiti (26).
Masengo alisema kutokana na elimu ambayo hutolewa na WMA kwa wakulima wa korosho na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kabla ya msimu, imesaidia kujua matumizi sahihi ya mizani.
Hatua hiyo imesaidia kupungua kwa tofauti ya uzito wa korosho unaotoka katika chama cha msingi na uzito unaopimwa kwenye ghala.
Pia, Masengo aliongeza kuwa hivi sasa wakala wa vipimo katika mkoa wa Pwani, unafanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye mizani inayopatikana kwenye vyama vya msingi na ile ya maghala makuu ili kujiridhisha kama walivyohakiki na kuziruhusu, zinapima kwa usahihi.
“Nawapongeza vyama vya msingi, wamejitahidi mizani nyingi tunakopita tunakuta ni sahihi na pale tunapogundua dosari ndogo ndogo zinafanyiwa marekebisho mara moja ili mkulima aendelee kupata faida ya jasho lake la kulima korosho,”alisema Masengo.
Kwa Mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura 340, Wakala wa Vipimo ndiyo yenye jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo vinavyotumika au vinavyotarajiwa kutumika kufanyia biashara kwa lengo la kumlinda muuzaji na mnunuzi.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, Stella Kahwa kutoka WMA Makao Makuu, alipongeza juhudi zinazofanywa na ofi si ya wakala wa vipimo mkoa wa Pwani.
0 comments:
Post a Comment