Musa Ally (25), mkazi wa Kiloleli wilayani Ilemela jijini Mwanza anayedaiwa kuwa na elimu ya chuo kikuu/shahada sayansi ya kompyuta aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) amejirusha katika jengo la la Rocky City Mall na kufariki dunia.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba 21, 2018 kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Advera Bulimba amesema tukio hilo limetokea leo saa saba mchana.
Imeelezwa kuwa Musa alichukua uamuzi huo kutokana na kuwa na msongo wa mawazo, kukosa kazi.
Bulimba amesema kijana huyo alionekana akiwa amelewa kupita kiasi na tangu Desemba 16, 2018 na alikamatwa na kuwekwa kituo cha polisi Kirumba, kilevi kilipopungua aliachiwa.
Amesema katika uchunguzi wa awali marehemu alibainisha kuwa alikuwa na msongo wa mawazo kwa sababu ya kukosa kazi licha ya kuwa na elimu ya juu.
Bulimba amesema baada ya polisi kumuachia alikwenda kunywa tena pombe na baadaye kujirusha kutoka ghorofa ya tatu na kukutwa na pombe kali na ugoro.
“Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa kijana huyo amesema amejiingiza kwenye ulevi na asilaumiwe mtu yeyote. Amesema amechukua uamuzi huo yeye binafsi, pia akidai yeye ni masikini hana baba wala mama,” amesema Bulimba.
Amesema mwili umehifadhiwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi licha ya kutotaja jina la hospitali hiyo.
Bulimba amesema, maandishi aliyokutwa nayo marehemu yalisomeka kwamba “yeye ana shahada sayansi ya kompyuta aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).”
Na Jonathan Musa na Jesse Mikofu, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment