Wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga Mkoani Mbeya wamesema kuungua moto kwa shule hiyo, kumewaathiri kimasomo baada ya shule kufungwa, ambapo baadhi yao walilazimika kupanga vyumba na kuishi maisha ya geto ili waendelee kujisomea.
Wakizungumza na Channel Ten wanafunzi hao, ambao wanataraji kuanza mtihani wao wa mwisho mwanzoni wa mwezi Mei, wanasema walishindwa kurudi nyumbani kwao kutokana na umbali na gharama za nauli kuwa kubwa, lakini pia wakawashukuru wadau waliojitokeza kuchangia shule hiyo na kwamba kwa sasa imekuwa kwenye hali nzuri tofauti na awali kabla ya kuungua moto.
Aidha, Afisa elimu Sekondari Lidya Halbert anasema uongozi wa shule umejipanga ambapo wanafunzi wa kidato cha sita baada ya masomo ya kawaida, watasoma masomo ya jioni ili kuziba pengo la siku ambazo hawakuwepo shuleni.
Hata hivyo wadau mbalimbali wameendelea kujitokeza kuisaidia shule hiyo, ambapo Benki ya Axcess tawi la Mbeya imetoa msaada wa mifuko 56 ya sement.
Shule hiyo ambayo iliungua moto mara mbili katika kipindi cha juma moja pia ina uhitaji wa vitanda 250, hivyo kuomba wadau mbalimbali kujitokeza kuisaidia shule hiyo.
0 comments:
Post a Comment