Shule mbalimbali za sekondari za bweni zinazomilikiwa na Serikali zimefungwa kutokana na kukosa chakula.
Uchunguzi umebaini takribani kwenye mikoa yote kuna shule zimefungwa na nyingine ziko hatarini kufungwa kwa kukosa chakula.
Mkoani Dodoma Shule ya Sekondari Mpwapwa iliyopo katika Wilaya ya
Mpwapwa ilitakiwa kufunguliwa tangu Aprili 8, lakini imeshindikana
kutokana na ukosefu wa chakula.
Mkuu wa shule hiyo, Nelson Mbilinyi, alisema walifunga shule kwa ajili
ya likizo fupi, lakini hadi sasa hawajajua ni lini watafungua kutokana
na tatizo hilo.
Mkoani Tabora, shule nne zimefungwa kutokana na wazabuni kusitisha
huduma kutokana na kuidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 1.5 za chakula
walichokisambaza kwa shule mbalimbali.
Sekondari zilizofungwa ni Kazima ambayo wanafunzi wote wamerudishwa
makwao isipokuwa wale wa kidato cha sita ambao wamepewa maelekezo ya
kuwa wavumilivu kwani watabaki wakijiandaa kwa ajili ya kufanya
mitihani.
Shule nyingine iliyofungwa ni Sekondari ya Tabora Boys ambapo kwa
mujibu wa mwalimu ambaye hakutaka kutaja jina lake, wanafunzi wote
wamerudishwa majumbani kwao na kubakishwa wa kidato cha sita tu
wanaojiandaa kwa mitihani yao ya mwisho.
Sekondari nyingine ambazo pia zimefungwa kutokana na kadhia hiyo mkoani
humo ni pamoja na Milambo na Tabora Girls ambazo idadi ya wanafunzi
waliorudishwa makwao haijafahamika.
Katika Mkoa wa Mtwara, taarifa zinasema shule za sekondari zilizopo wilayani Masasi tayari zimefungwa kutokana na hali hiyo.
Shule hizo zimetajwa kuwa ni Ndanda Boys, Masasi Girls, Chidya na Ndwika.
Katika Mkoa wa Mwanza, wazabuni wa vyakula mashuleni wametishia kugoma
kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh milioni 800.
Shule ya Sekondari Mwanza, iliyopo katika Wilaya ya Nyamagana inadaiwa
na mzabuni kiasi cha Sh milioni 116, ambazo ameshindwa kulipwa kwa
kipindi cha miaka miwili mfululizo.
Shule nyingine ambazo zinadaiwa na wazabuni ni Sekondari yaNsumba pamoja
na Ngaza, ambapo taarifa za uhakika zinaeleza kuwa kwa ujumla wake
zinadaiwa zaidi ya Sh milioni 300.
Mkoani Arusha nako hali si shwari baada ya shule za Ilboru, Longido,
Engutoto, Makuyuni na Kisimiri kudaiwa kuwa katika hali mbaya kutokana
wazabuni kudai mamilioni ya fedha.
Mkoani Mbeya, Shule ya Sekondari ya Iyunga, inatarajiwa kufungwa leo, kutokana na ukosefu wa chakula.
Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Edward Mwakimwa, alikiri kukabiliwa na uhaba
wa chakula na kusema tayari uongozi wa shule kwa kushirikiana na
Serikali ya Mkoa unaendelea na mchakato wa kuhakikisha chakula
kinapatikana kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment