Askari
lazima atishe. Popote anapokuwapo
wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari
dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu
utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache
wanaoendelea na vitendo hivyo." Omari Mahita
Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Omary Mahita amesema askari polisi kwa
sasa wamepoteza hadhi, hawaogopwi na wahalifu na ndiyo sababu kubwa ya
kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu kila kukicha.
Mahita
aliyestaafu mwaka 2006, alisema mbali na kuongezeka kwa uhalifu,
inafikia hatua wahalifu wanawaingilia polisi kwa kuvamia vituo vya
polisi na kupora silaha ilhali zamani hakukuwa na matukio hayo.
Hata
hivyo, IGP, Ernest Mangu amejibu kauli hiyo akisema: "Siwezi kutumia
mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa anakabiliana nacho, kwa sasa
hakipo.
Kauli ya Mahita
Kauli ya
Mahita imekuja miezi minane baada ya askari 10 kuuawa na bunduki zaidi
ya 20 kuporwa katika matukio mbalimbali ya uvamizi wa polisi na vituo
vya polisi.
Akizungumza
na mwandishi wetu baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa
Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Dk Mohamed Mhita,
Oysterbay Dar es Salaam juzi, Mahita alisema: "Ili kupunguza vitendo vya
kihalifu vinavyozidi kuongezeka kila kukicha, ni lazima askari
warudishe hadhi yao ya kuogopwa na wahalifu popote walipo.
"Askari
lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari
dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu
utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache
wanaoendelea na vitendo hivyo."
Mahita
alikosoa kitendo cha askari polisi kuwa wapole na kueleza kuwa hilo ni
suala lisilotakiwa kabisa kufanywa ndani ya jeshi hilo na polisi...
"Unambembelezaje mhalifu? Hawa ni watu wanaostahili kubanwa kwa kila
namna ili kukomesha vitendo vyao katika jamii. Mhalifu yeyote akiachiwa,
madhara yake ni makubwa katika jamii."
Licha ya
suala hilo, IGP huyo mstaafu alieleza umuhimu wa doria katika kudhibiti
uhalifu wa kila siku ambao hupunguza amani miongoni mwa jamii na
kuwafanya wananchi washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na
ratiba waliyojiwekea.
Alitolea
mfano wa vikundi vya uhalifu vilivyojitokea hivi karibuni kama 'Panya
Road', 'Mbwamwitu' na 'Libya' kwamba vimekuwapo kutokana na kupungua kwa
doria inayotakiwa ifanywe na jeshi hilo nchi nzima na hasa maeneo ya
mijini.
"Enzi
zangu doria ilipewa kipaumbele. Magari na pikipiki yalikuwa yanazunguka
kote katika jiji hili na kwingineko mikoani karibu kila siku na walikuwa
wanaogopeka... kwa sasa yapo lakini sidhani kama wanafanya kazi kama
ilivyokuwa enzi zile," alisema Mahita.
"Wahalifu
walikuwa wanajua kuwa polisi wapo kazini muda wote. Lakini sasa hivi
mambo hayo hayapewi uzito unaotakiwa ndiyo maana unaona kikundi kama
Panya Road kinatingisha mji mkubwa kama huu (Dar es Salaam).
0 comments:
Post a Comment