Rais John Magufuli ameshauriwa ‘kulegeza’ kidogo demokrasia ili Watanzania wapate afueni kutokana na sasa kujaa hofu.
Akizungumza kwenye kikao kati ya Rais Magufuli na viongozi wa dini leo Jumatano tarehe 23 Januari 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Lyimo amesema, hata kama haambiwi ukweli ni kwamba, Watanzania wana hofu.
“Mhe. Rais, unafanya kazi nzuri sana lakini baba demokrasia, Watanzania wengi wana hofu, hata kama huambiwi na watendaji wako.
“Wengi hawathubutu kuzungumza kwa kuwa wana hofu. Kwa hiyo kama kunauwezekano baba waachie pumzi kidogo wazungumze,” amesema Mchungaji Aman Lyimo.
Ingawa Askofu Lyimo hakutaja kundi alilokusudia kwamba linabanwa lakini maelezo yake yaliyofuata yalionesha kukusudia wanasiasa.
“Watanzania hawatachagua maneno bali watachagua utendaji kazi. Kwa kuwa wewe ni mchapa kazi, watachagua kazi zako badala ya maneno,” amesema Askofu Lyimo.
Via Mwanahalisionline