Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Zuberi Homera akiwa nyumbani kwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho marehemu Jenista Mhagama Makambi Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Juma Zuberi Homera, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, ameitembelea familia ya marehemu Jenista Mhagama nyumbani kwake Makambi, Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, na kutoa pole kufuatia msiba wa aliyewahi kuwa Mbunge na Waziri mstaafu.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri amepata wasaa wa kusaini kitabu cha maombolezo na kutoa salamu za pole kwa familia, ndugu na waombolezaji waliokuwepo.
Amewapa moyo wa kuendelea kuwa imara katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na kuwataka waendelee kushikamana.
Akiwa nyumbani hapo, Mheshimiwa Dkt. Homera ameeleza masikitiko yake makubwa kufuatia msiba huo na kutambua mchango mkubwa wa marehemu Jenista Mhagama katika kulitumikia Taifa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Aidha, amewahimiza waombolezaji kuendelea kuwa na subira, mshikamano na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema.
Ikumbukwe kuwa Mheshimiwa Waziri hakupata fursa ya kuhudhuria mazishi ya marehemu kutokana na majukumu ya kikazi jijini Nairobi, nchini Kenya, ambako alikuwa akiongoza kikao cha 11 cha Mawaziri wa Sheria na Haki wa Umoja wa Afrika na kurejea nchini disemba 18 ,2025.

0 comments:
Post a Comment