Na Christina Haule, Morogoro
MTANDAO wa wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) unafanya juhudi za kuongeza 00pushirikiano ya kiuchumi na kijamii kati ya nchi yetu na mataifa makubwa kama vile China na Brazil ili kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa wingi na kunufaika kutokana na jasho lao kupitia masoko yenye tija.
Hayo yameleezwa mjini Morogoro na Mkurugenzi MVIWATA, Stephen Ruvuga, wakati akitambulisha taasisi ya Mashirikiano ya kimataifa Baobab kutoka nchini Ghana na Brazil na taasisi ya Gorduana kutoka nchini China.
Anasema MVIWATA na mashirika hayo wanajadiliana namna ya wakulima wa mazao mbali mbali ikiwemo kahawa wanaweza kuzalisha kwa wingi na kunufaika moja kwa moja kutoka kwa wanunuzi.
Anasema ushirikiano huo utaendelea kuwa mkombozi kwa kuhakikisha maisha ya wakulima wadogo yanakuwa bora zaidi kwa kuwezesha upatikanaji wa pembejeo na masoko ya mazao ya kimataifa yenye tija.
Aidha Ruvuga alisema ujio wa taasisi hizo kubwa mbili umelenga kuanzisha ushirikiano kati ya wakulima wadogo wa hapa nchini hususani wanachama wa MVIWATA na wakulima na taasisi nyingine kutoka nchi za Ghana, Brazil na China na kuboresha suala la kilimo nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utambulisho Mkurugenzi wa taasisi ya Gorduana, kutoka nchini China, Jit Zhou, alisema kuna mahitaji makubwa ya kahawa nchini humo.
“ China ni nchi yenye idadi kubwa ya watu, na awali hakukuwa na watumiaji wengi wa kahawa, kwa sasa idadi ya watumiaji wa kahawa nchini humo imeongezeka sana, hivyo bidhaa hiyo inahitajika kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya watumiaji. Alisema Zhou.
Naye Katibu Mkuu wa kampuni ya Baobab, Kyeretwice Opoku kutoka nchini Ghana alisema kuwa taasisi yake imepanga kushirikiana na wakulima wa Tanzania kupitia MVIWATA ili kuwezesha upatikanaji wa teknolojia ya kilimo na kuwafundisha wakulima kuzalisha mazao kwa kutumia mbolea za asili zisizo na kemikali huku mkazo mkubwa ukiwa ni kuchechechemua uzalishaji wa mazao mbali mbali ikiwemo kahawa.
Akizungumza kuhusu fursa hiyo kwa wakulima, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rose Rwegasira, alisema ujio wa mashirika hayo utasiadia kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao kwa kuwa kutaongeza upatikana wa pembejeo za kilimo na masoko.
0 comments:
Post a Comment