Wananchi wa kijiji cha Bujika Kata ya Nyandekwa katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamefanikiwa kumuua mnyama aina ya Fisi aliyewaua mbuzi sita usiku wa kuamkia leo Disemba 03, 2021.
Fisi huyo alivamia banda la Mbuzi wa Mzee Keneth Shaban majira ya saa tano usiku na kuwashambulia Mbuzi waliokuwa ndani ya banda hilo ambapo imeelezwa kuwa baada ya fisi huyo kuingia katika banda hilo mlango ulijifunga na kushindwa kutoka.
Akizungumzia tukio hilo Afisa Maliasili msaidizi wa Manispaa ya Kahama, Thomas Manumbu amesema baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na walikuta tayari wananchi wamemuua fisi huyo ambapo mbali na kuua Mbuzi hao hakuna mtu aliyethurika.
"Tulipata taarifa kutoka kwa katibu tawala kuhusiana na tukio hilo ni kweli limetokea lakini halidhuru mtu yoyote kikubwa tu limesababisha Mbuzi hao kuuliwa na mnyama huyo",amesema.
Hata hivyo amewataka viongozi wa serikali za vijiji na kata kuimarisha kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao ili kukabiliana na wanyama hao ambao wamekuwa wakisababisha madhara kwa binadamu pamoja na mifugo.
CHANZO- HUHESO FM
0 comments:
Post a Comment