NA MWANDISHI MAALUM, MADRID, HISPANIA
UJUMBE wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro upo nchini Hispania, katika Jiji la Madrid kushiriki mkutano mkuu wa 24 wa Kimataifa wa Utalii Duniani ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Utalii Duniani ( UNWTO)
Katika mkutano huo wa siku nne ulioanza jana, unaotarajiwa kufunguliwa rasmi leo hii Desemba Mosi, ambapo Waziri Ndumbaro akiwa katika jiji hili la Madrid, ameweka bayana mambo mbalimbali ambayo Tanzania itanufaika na mkutano huo.
Akizungumzia mambo hayo, Dkt. Ndumbaro amesema ''katika kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watalii kuitembelea Tanzania pamoja na mapato yatokanayo na Utalii, suala la kutangaza utalii wa Tanzania katika nyanja za kidunia ni suala ambalo haliepukiki ''
Ametaja moja ya kati ya maeneo ya kutangaza Utalii huo, ni kuhudhuria mikutano mikubwa duniani ambayo Inahusisha masuala ya Utalii ikiwemo kuja nchini Hispania ambako ndiko makao makuu ya utalii Duniani katika jiji la Madrid, kwa ajili ya kuhudhuria mkutano mkuu huu wa 24.
Ikiwa ni siku ya kwanza ya mkutano huo Tanzania ilipata fursa kadhaa ikiwemo kutumia mkutano huu kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania, kuwaambia dunia nzima kwamba Tanzania ipo salama na kuwataka watalii kuja kujionea vivutio vya utalii ilivyonanvyo
''Waje Tanzania wauone Mlima Kilimanjaro, waje Tanzania waione Serengeti, waje Tanzania waione Ngorongoro, waje Tanzania waone fukwe nzuri zenye mchanga mweupe zilizopo Zanzibar, waje Tanzania waone vivutio mbalimbali ambavyo tupo navyo.’’ Alisema Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa, katika suala la pili katika mkutano huo, Tanzania itasaini mkataba na UNWTO wa kuweza kuwa mwenyeji wa mkutano wa 65 wa Utalii Barani Afrika ambao utafanyika kati ya tarehe 6-8 Oktoba 2022 katika jiji la Arusha.
‘’Mkutano huu tunauleta kwa sababu ni fursa nyingine kwa Tanzania, Tulishapewa kuwa mwenyeji wa mkutano wa utalii wa kanda ya Afrika kule nchini Cape verde, lakini sasa tumekuja kusaini makubaliano ya kuwa wenyeji wa mkutano huo, baada ya kusaini sasa tutakuwa na uhakika asilimia 100 na tumetengeneza ‘Post card’ ambapo kila mshiriki aliyekuja hapa tunampa post kadi hizi ambayo inasaidia sana kutangaza utalii wa Tanzania.’’ Alisema Dkt. Ndumbaro.
Aidha, alisema kuwa suala la tatu kwenye mkutano huo, Tanzania imekuwa katikak mstari wa mbele kupigania haki za Watalii ambapo watashiriki katika kufanikisha sheria ya Kimataifa inapitishwa.
‘’Jambo lingine ambalo tunalifanya katika mkutano huu, ni kupitisha sheria ya kutetea haki za watalii duniani pale inapotokea matatizo.. tumejifunza kutokana na kadhia ya UVIKO 19 kwamba nchi zilifunga mipaka, na baada ya nchi kufunga mipaka , watalii walikuwa wapo kwenye nchi zingine na hawaweza kurudi.
‘’Sasa haki zao zilikuwa haziwezi kutetewa na sheria za kimataifa. Kwa hiyo sasa tunapitisha sheria ya kimataifa ya kutetea watalii katika mazingira ya dharura kama hayo. Ni sheria ambayo itaongeza heshima ya baishara ya utalii duniani, kwa sababu unapolinda haki ya mtalii, mtalii anajiona yupo salama zaidi kuja na kushiriki katika nchi yako, Tanzania tumekuwa mstai wa mbele kuhakikisha sheria hiyo inapita.’’ Alisema Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro alisema kuwa, mkutano huo una faida nyingi sana kwa nchi Tanzania, katika kuhakikisha kwamba tunatimiza idadi ya watalii milioni tano na mapato zaidi ya bilioni sita.
‘’Tunatumia mkutano huu kama fursa ya sisi kuweza kutangaza utalii, lakini kama fursa ya kuwavuta wenzetu waje pia, tumepongezwa kwa namna ambavyo tumeweza kufanya onesho la kwanza la utalii katika nchi za Afrika Mashariki. Sisi tuliona dogo, lakini wenzetu huku katika nyanja za kimataifa tumepongezwa na nimesema kwamba kumbe kweli watanzania wanaweza kufanya mikutano kwa kiwango kikubwa zaidi’’ alisema Dkt. Ndumbaro.
Mkutano huo wa 24 wa Kimataifa wa Utalii duniani, ni wa siku nne, kuanzia jana Novemba 30 hadi 3 Desemba, ukijumuisha ujumbe mbalimbali wakiwemo Mawaziri wa Utalii, viongozi wakuu wanchi, Mashirika ya Kimataifa ya Serikali, binafsi, wadau wa Utalii na watu mbalimbali waalikwa.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment