Thursday, 2 December 2021

Freeman Mbowe na Wenzake Wafunga Ushahidi....Uamuzi wa Kesi Ndogo ndani ya Kesi ya Msingi Kutolewa Disemba 14

...


Mahakama  Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar ea Salaam, imepanga kutoa uamuzi wa kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya yapokelewe au la tarehe 14 Desemba 2021.

Ni baada ya upande wa utetezi katika kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, watatu.

    Tarehe hiyo imepangwa janaJumatano, tarehe 1 Desemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, baada ya upande wa utetezi kuomba kufunga ushahidi wake katika kesi hiyo ndogo.

Katika kesi hiyo, upande wa utetezi ulipinga maelezo hayo ya onyo yasipokelewe kwa madai si halali kwa mujibu wa sheria kwani hayakutolewa na mshtakiwa huyo.

Jaji Tiganga ameelekeza mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha mawasilisho yao kwa njia za maandishi tarehe 7 Desemba 2021, ili kuandaa uamuzi dhidi ya kesi hiyo kama mahakama hiyo iyapokee maelezo ya onyo au isiyapokee.

Wakili wa Ling’wenya ambaye ni mshtakiwa wa tatu, Fredrick Kihwelo, aliomba wafunge ushahidi baada ya shahidi wao wa tatu, Gabriel  Mhina, kumaliza kutoa ushahidi wake.

Mhina ambaye alikuwa ni Komandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alianza na kumaliza kutoa ushahidi wake jana, ambapo aliieleza mahakama hiyo namna alivyoingizwa kwenye kesi hiyo na kisha kuachwa huru kabla haijahamishiwa mahakani hapo ikitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Alidai, aliachiwa huru  baada ya Mbowe kukamatwa na kwamba upande wa mashtaka ulidai hauna nia ya kuendelea naye katika kesi ya uhujumu uchumi namba 63/2020 iliyokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Pia, Mhina alidai baada ya kukamatwa mkoani Tabora tarehe 19 Desemba 2020, alipatiwa mateso kwa kupigwa na kufungwa pingu muda wote. Pia alidai askari polisi waliomkamata hawakumuonya juu ya kosa lililokuwa linamkabili na wala hawakuandika taarifa zake katika kitabu cha kumbukumbu za mahabusu, katika vituo vya polisi alivyofikishwa.

Mbali na Mhina, mashahidi wengine wa utetezi walikuwa ni Ling’wenya mwenyewe aliyedai kwamba maelezo ya onyo yaliyoletwa mahakamani hapo na upande wa jamhuri hakuyatoa bali alilazimishwa kuandika nyaraka iliyodaiwa kuwa na maelezo hayo.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger