Na Mwandishi Wetu, SUMBAWANGA
KLABU ya Simba imehitimisha msimu wake mzuri baada ya kutwaa taji la tatu kufuatia kuichapa Namungo FC mabao 2-1 katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzana (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) jioni ya leo Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.
Simba SC ilifungua msimu vizuri kwa kubeba Ngao ya Jamii kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya waliokuwa mabingwa wa ASFC, Azam FC Agosti 17, mwaka jana Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam na wiki mbili zilizopita ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo.
Dalili za Simba kubeba taji lingine leo zilianza mapema tu dakika ya 27 baada ya nyota kutoka Msumbiji, Luis Jose Miquissone kufunga bao la kwanza akimalizia mpira uliookolewa na beki Carlos Protas kufuatia krosi ya beki wa kulia Shomari Salum Kapombe.
Na ni wakati huo Simba ilipata pigo kidogo, baada ya kiungo wake Mkenya, Francis Kahata Nyambura kushindwa kuendelea na mchezo kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na mzawa, Hassan Dilunga aliyekwenda kuziba vyema pengo hilo.
Nahodha John Raphael Bocco akaifungia bao la pili Simba SC dakika ya 39 kwa kichwa cha kudundisha akimalizia pasi ya kichwa ya mchezaji wa zamani wa UD Songo ya kwao, Msumbiji Miquissone kufuatia krosi maridhawa ya kiungo Mzambia, Clatous Chotta Chama kutoka upande wa kulia.
Beki wa zamani wa Yanga SC, Edward Charles Manyama akaifungia Namungo FC bao la kufutia machozi dakika ya 56 akimalizia kona ya kiungo Abeid Athumani kutoka upande wa kulia.
Miquissone aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mamelodi Sundowns ambayo ilimpeleka kwa mkopo klabu yake ya zamani, UD Songo alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi baada ya mchezo huo Chama akachaguliwa Mchezaji Bora wa Mashindano.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Gerson Fraga ‘Viera’, John Bocco, Clatous Chama na Francis Kahata/Hassan Dilunga dk27.
Namungo FC; Nourdine Balora, Rodgers Gabriel, Edward Manyama, Steven Duah, Carlos Protas, Hamisi Khalfan, Hashim Manyanya/Frank Mkumbo dk60, Daniel Joram/Steven Nzigamansabo dk46, Bigirimana Blaise, Lucas Kikoti na Abeid Athumani.
Chanzo- BINZUBEIRY BLOG
0 comments:
Post a Comment