Monday 31 August 2020

WAZAZI WAFURAHIA KUWEPO MABASI YA KUTOSHA WATOTO WAO

...

 
Mfano wa Basi la shule

Na Abby Nkungu, Singida
TATIZO la wanafunzi  shule  za  mchepuo wa  Kiingereza (English Medium) kuchelewa kuchukuliwa kwenda shuleni  na kurejeshwa  nyumbani katika Manispaa ya Singida sasa limebaki historia baada ya  Serikali kuchukua hatua mbalimbali; ikiwemo kuwataka wamiliki wa Taasisi hizo kuwa na mabasi ya  kutosha.


Mwandishi wa habari hizi amebaini kuwa baada ya  janga  la Corona kupungua na  shule  kufunguliwa, Serikali  iliwahimiza  wamiliki wa shule hizo kuwa na mabasi ya kutosha kuepuka msongamano wa watoto wanapokwenda shuleni na kurejea  nyumbani ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia kusambaa zaidi  kwa  maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Awali, baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma kutwa katika shule hizo walilalamika kwenye majukwaa mbalimbali watoto wao  kulazimika kuamka saa 11:00 alfajiri kila siku za masomo kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule na kuchelewa kurejea nyumbani hadi  saa 2:00 usiku.

Walisema kuwa  hali hiyo ilikuwa ikileta adha kubwa  kwa mtoto wa shule za awali mwenye umri wa chini ya miaka sita kulazimika kuamka mapema  alfajiri na kurejea usiku; hivyo  kuchoka na kusababisha achukie shule kwa kuona kama vile ni adhabu.

Ilielezwa kuwa moja ya sababu kuu iliyochangia watoto wao kuamka mapema ni uhaba wa mabasi ya shule hizo; hivyo gari moja kulazimika kuanza mzunguko wa kuwachukua  watoto mapema alfajiri kuwapeleka shule ili kurudi kuchukua wengine. Vivyo hivyo, wakati wa kuwarejesha nyumbani jioni.

“Tunashukuru Mungu baada ya kupiga kelele kupitia vyombo  vya  habari, Serikali ikasikia na kuwabana wamiliki  wa shule.  Wengi wao wameongeza magari sasa mtoto anaweza kuamka saa moja akajiandaa na kurejeshwa saa 11 jioni” alisema  Halima Njiku mkazi wa Kibaoni mjini Singida.

“Janga la Corona limetusaidia sana, watoto hawapakatiani tena kwenye viti kwani shule nyingi zimeongeza magari  kuepuka  kufungiwa; hivyo kilio chetu  cha muda mrefu  kupitia vyombo vya habari kimesikika...tunashukuru” alisema  mzazi  mwingine, Juma Omari mkazi  wa Mwenge  mjini hapa.

Ofisa elimu Taaluma shule za Msingi Manispaa ya Singida, Gerson Mrua alisema baada ya  malalamiko ya wazazi na walezi, waliamua kuwaandikia barua wamiliki  wote  wa shule  hizo za English Medium kuwataka  wawe na magari ya  kutosha  kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma kutwa.

“Lakini pia tuliwaagiza warekebishe ratiba zao za kuwachukua asubuhi na kuwarejesha jioni wanafunzi ili kupunguza adha kwa wazazi, walezi na watoto pia" alisema  Ofisa  huyo.

Wataalam wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto wanasema mtoto anapaswa kupumzika  angalau kwa saa moja hadi mbili awapo shuleni na kwa shule zinazokaa na watoto kwa muda mrefu zaidi lazima ziwe na ratiba yenye huduma ya mapumziko; ikiwemo kulala kwa muda kwa kuwa kupumzika ni afya kwa mtoto kwani ubongo wake bado unakua kwa kasi.  MWISHO
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger