Thursday 27 August 2020

Matamko ya mitandaoni yatahadharishwa kuwaponza wapiga kura

...
Na Samirah Yusuph
Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu limewatahadharisha wananchi kuepuka matamko ya mitandaoni yatakayo pelekea uvunjifu wa amani wakati huu wa uchaguzi.

Akitoa angalizo hilo kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu SACP Henry Mwaibambe amewataka wananchi kuepuka kujihusisha na usambazaji wa taarifa zisizo na ukweli na kuzifanyia kazi kwani vitendo hivyo ni ukiukaji wa sheria na polisi hawatasita kuwachukulia hatua kwakuwa taarifa hizo zinaweza kuvuruga amani wakati huu wa kampeni za uchaguzi na kuwataka wananchi kupata taarifa sahihi za kiusalama kutoka katika jeshi la polisi pekee.

“mikutano yote itakuwa na usimamizi wa jeshi la polisi, kuna uvumi umekuwa ukisambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu vitendo vya uhalifu mkoani hapa jambo ambalo ni uongo, mkoa wetu hauna matukio ya uvunjifu wa amani,tumejipanga vizuri kwa kufata sheria ya nchi,” alisema Mwaibambe.

Aidha amewatahadharisha wananchi kuhusu kujichukulia sheria mkononi kwa kushiriki vitendo vya vitakavyo wapelekea kuwa hatarini na kuwataka kutoa taarifa wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

Jambo ambalo limewekewa mkazo na kaimu kamishina wa fedha na lojistiki DCP Dhahiri Kidavashari alipokuwa akikaguwa utayari wa jeshi la polisi mkoani hapo na kueleza kuwa kuna matamko yanayotolewa na baadhi ya wagombea ambayo hawawezi kuyavumilia.

DCP Kidavashari alisema matamko hayo hawawezi kuyapa nafasi ili kuvuruga amani, na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano  katika viashiria hivyo ili kuhakikisha polisi wanafanya kazi yao ili kudhibiti uvunjifu wa amani.

“Adhima ya nchi yetu ni uchaguzi unatakiwa uwe huru, haki na amani itawale, sisi kama jeshi la polisi tumejipanga ili kuhakikisha kwamba adhima hii inatimia na kuanzia kampeni hadi matokeo kutangazwa amani itawale,” alisema Kidavashari.

Aliongeza kuwa jeshi la polisi lipo tayari kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na kila mmoja anapiga kura kama inavyotakiwa na kwamba atakayetenda jema atapokea zawadi na atakayetenda vibaya kiboko kitamfata hivyo inabidi wawe makini.

Kampeni za uchaguzi mkuu  unaotarajiwa kufanyika octoba 28 mwaka huu zimezifunguliwa leo kote nchini ambapo wagombea wanapata nafasi ya kunadi sera zao kwa muda wa siku 63.

Mwisho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger