Saturday 8 August 2020

Serikali Yabuni Mbinu Ya Kubaini Viuatilifu Feki-Waziri Hasunga

...
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Licha ya kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kuendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuongeza upatikanaji wa mbegu na viuatilifu bado wapo wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoingiza pembejeo hizi feki katika maduka yao na kuwabambikizia wananchi.

Ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara ya mbegu wasio waaminifu hawaingizi sokoni mbegu feki, taasisi za TOSCI na TTCL zimebuni mfumo wa kielektroniki utakao wawezesha wakulima kubaini mbegu feki zilizo na lebo feki.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga jana  tarehe 7 Agosti 2020 wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma maalum ya kuhakiki pembejeo za kilimo inayojulikana kama T-Hakiki wakati wa sherehe za wakulima (Nanenane) katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Aidha, ili kudhibiti ubora wa viuatilifu, Waziri Hasunga amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2019/2020, Wizara kupitia TPRI imekagua wafanyabiashara 222 wakiwemo wauzaji, watengenezaji, wafukizaji na waagizaji kutoka mikoa saba nchini.

Pia TPRI imetoa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu kwa wakulima, maafisa ugani na wauzaji 765 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuendeleza jitihada za kudhibiti matumizi ya viuatilifu feki.

Vivyo hivyo, Wizara kupitia TOSCI na sekta binafsi inaendelea kuimarisha upatikanaji, utumiaji na udhibiti wa mbegu ili kuongeza tija, kipato na usalama wa chakula na lishe.

Amesema kuwa kutokana na kukua kwa sekta ya mbegu nchini, matumizi ya mbegu bora zilizothibitishwa na TOSCI yameongezeka kutoka tani 10,946 (2014/2015) hadi tani 57,023 (2018/2019).

Mhe Hasunga amesema kwa katika juhudi hizo za kuongeza matumizi ya mbegu bora, Wizara kupitia TOSCI imeongeza kiasi cha mbegu bora zilizothibitishwa na TOSCI zinazozalishwa hapa nchini kutoka tani 4,337 (2014/2015) hadi tani 46, 335 ambazo ni asilimia  81 ya mbegu zote zilizothibitishwa na TOSCI.

Kadhalika, ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na udhibiti wa ubora wa mbegu, Wizara kupitia TOSCI imekuwa ikiongeza matumizi ya lebo za ubora za TOSCI. “Katika mwaka wa fedha 2019/2020, jumla ya lebo 9,000,000 zilitolewa na TOSCI kwa wazalishaji mbali mbali wa mbegu ikilinganishwa na lebo 400 zilizotolewa mwaka wa fedha 2014/2015” Amekaririwa Mhe Hasunga

Hasunga amesema kuwa mfumo wa T-hakiki, ni sawa na mkombozi kwa mkulima kwa sababu ni huduma inayomwezesha mkulima kupata taarifa ya mbegu na kiuatilifu kilichosajiliwa.

“Pia inamsaidia mkulima kufahamu matumizi sahihi ya pembejeo hizo kupitia simu ya mkononi, hakika haya ni mapinduzi bora ambayo yatazidi kumkomboa mkulima lakini pia kuisaidia Serikali kukabiliana na wafanyabiashara wasio waaminifu na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima wetu” Amesisitiza Waziri Hasunga

MWISHO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger