Saturday, 8 August 2020

Manyanya Ataka Tume Ya Uchaguzi Kuchukua Hatua Kwa Wacheza Faulo

...
Na Mwandishi wa NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetakiwa kuchukua hatua inapoona faulo za wazi wazi hasa wakati huu ambapo michakato mbalimbali ya uchaguzi inaendelea nchini.

Tayari Fomu za Uteuzi Kwa nafasi ya wanaogombea Kiti cha Rais zimeanza kutolewa tangu Agosti 5 hadi 25 mwaka huu na kwa upande wa Ubunge na Udiwani fomu za uteuzi kwa wagombea  zitaanza kutolewa Agosti 12 hadi Agosti 25, mwaka huu.

Akizungumza kwenye banda la NEC jana kwenye maonesho ya wakulima yanayofanyika katika viwanja vya nane nane Nzuguni Jijini hapa, Naibu Waziri wa Viwanda Injinia Stella Manyanya alisema kazi kubwa inayofanywa na tume imekuwa ikionekana hasa katika michakato ya uchaguzi kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

” Kazi kubwa inafanyika lakini kazi iliyo mbele ni ngumu kwani kuna watu wanagombea kwa kufuata taratibu lakini wengine sivyo, kuna maneno ya hovyo hovyo, kuchafuana  hata kabla ya kuchukua fomu za uteuzi mambo mengi yanaonekana, mkiona faulo za wazi wazi mchukue hatua hata vyombo vya sheria vichukue hatua ili uchaguzi uwe wa haki,” alisema

Alisema pia kuna haja ya kuhakikisha elimu wanazotoa zinawafikia wananchi waliopo vijijini na kuweka mazingira ya kupata elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo wajasiriamali na makundi maalum ikiwemo walemavu.

Alisema, taifa linakwenda kufanya maamuzi magumu kwa kuchagua kiongozi anayefaa kuliongoza taifa.

“Taifa linakwenda kufanya maamuzi magumu ya nchi yetu sio maamuzi ya mtu ni maamuzi ya hatma ya taifa, tukachague kiongozi mwenye mapenzi mem ana nchi yetu atakayelifanya taifa lizidi kusonga mbele,” alisema.

Alisema kila mmoja anatakiwa kuzingatia kanuni na taratibu na wananchi wasikubali kutumika na kikundi chochote kwa kufanya mambo yanayohatarisha amani.

Alivitaka vyama vya siasa kuheshimu sheria za nchi ili uchaguzi ufanyike kwa haki na amani.

“Uchaguzi ni wakati wa kufanya maamuzi sahihi,” alisema

Pia alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwe na tume huru ya uchaguzi.

“Tume iliyopo ni huru, twende kwenye uchaguzi sasa,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Idara ya Habari na Elimu kwa Mpiga Kura, Johari Mutani alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi wamejipanga katika maandalizi ya uchaguzi.

“ Tulifanya uboreshaji wa daftari awamu ya kwanza, kisha awamu ya pili, ucjakataji wa taarifa za daftari ukawa unaendelea sasa tume itaanza kutoa fomu kwa wagombea wa Ubunge na Udiwani Agosti 12, mwaka huu,” alisema.

Alisema wanawafikia wananchi kwa kutoa elimu kwa njia mbalimbali, ikiwemo matangazo, vipindi vya redio, blogs na kuweza kukutana moja kwa moja na wapiga kura.

Kwa Mujibu wa Ratiba iliyotolewa na NEC, Uchaguzi wa Rais Wabunge na madiwani utafanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Fomu za uteuzi kwa wagombea wa kiti ya Rais na Makamu wa Rais zitaanza kutolewa Agosati mosi hadi Agosti, 25 mwaka huu katika ofisi za NEC Njedengwa Jijini Dodoma.

Pia fomu za uteuzi kwa wagombea ubunge zitaanza kutolewa Agosti 12 hadi Agosti 25 mwaka huu katika ofisi za halmashauri husika.

Fomu za uteuzi kwa wagombea udiwani zitaanza kutolewa Agosti 12 hadi Agosti 25 katika ofisi za kata husika.

Aidha uteuzi wa wagombea kiti cha Rais,  Makamu wa Rais, Ubunge na Udiwani utafanyika Agosti 25, mwaka huu.

Kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 26 na hadi Oktoba 27, mwaka hu una Oktoba 28, mwaka huu itakuwa siku ya uchaguzi Mkuu.

Mwisho


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger