Wednesday, 12 August 2020

Dkt.Abbasi atoa ufafanuzi kuhusu Kanuni za Maudhui Mtandaoni

...
Na Eleuteri Mangi – WHUSM, Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema mambo yote yanayohusu maudhui ya utangazaji katika Redio, Televisheni na Mitandao ya Jamii Wizara yenye dhamana na habari ndiyo inawajibika.

Dkt. Abbasi amesema hayo jana Jijini Dar es salaam alipokuwa katika mahojiano maalum Global TV Online kuzungumzia Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano ambapo alisema Kanuni za Mtandaoni zinasimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Kuna mambo yanahitaji uelewa, Kanuni za Maudhui Mtandaoni ni za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kimfumo na maudhui yanasimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo” alisema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi alifafanua kuwa kwa mujibu wa Muundo wa Kisera, TCRA inawajibika katika Wizara mbili kisekta ambapo masuala ya mawasiliano upande simu, mitambo ya simu, kutoa leseni za makampuni ya simu, eneo hilo linasimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Akiendelea kuzungumza Dkt.Abbasi alisema TCRA inamuunganiko kati ya mitambo na maudhui, na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo inasimamia maudhui ya tasnia ya habari zinazosambazwa kupitia vyombo vya habari ikiwemo Redio, Televisheni na Mitandao ya kijamii nchini.

Kwa mujibu wa Sheria ya TCRA ya 2003, EPOKA 2010 na mabadiliko yake inamtamka Waziri anayehusika na maudhui ni Waziri wa Habari na sheria imetoa utaratibu wa kutunga kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo kwa muktadha wa utawala bora kwa kuwashirikisha wadau wanaohusika katika kutekeleza sheria hiyo.

Pamoja na hayo Dkt. Abbasi alifafanua kuwa TCRA wamefanya kazi yao ya kuwashirikisha wadau na wakaleta Wizarani maoni hayo waliyoyakusanya, sisi wenyewe kama wadau tulitoa maoni yetu kwa sababu walianza na wadau wao halafu wakaja kwenye ngazi ya Wizara husika.

“Nakumbuka Mhe. Waziri wakati TCRA wanawasilisha kwa mara ya kwanza Kanuni hizo wizarani alisema pamoja na maoni mliyokusanya, rudini tena kwa sababu kulikuwa na maoni mapya ambayo wadau hawakuyajadili na mpaka wengine waliandikiwa barua kutoa maoni yao kwa maandishi,” alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, katika Mahojiano Maalum na Global TV, Dkt. Abbasi alijibu swali aliloulizwa kuhusu wanafunzi wa taaluma ya habari kupewa vitambulisho (Press Card) alisema Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za 2017, 18(1) inaruhusu wanafunzi wa taaluma ya habari kupata vitambulisho vya wanahabari ili iwasaidie wasipate shida na wafanye kazi kwa weledi wakati wakiwa katika mafunzo kwa vitendo.

Kwa upande wa Sekta ya Michezo, Dkt. Abbasi amesema wajibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) unapaswa kuwa mkubwa kuliko sasa, ni lazima uwepo mifumo unayohakikisha inakomesha masuala ya ujanja ujanja kwenye usajili pamoja na masuala ya kuingiza wachezaji wa kigeni yanakaa vizuri.

Kuhusu mpango endelevu wa kuinua vipaji vya michezo kuanzia chini, hivi karibuni Serikali inakuja na mkakati wa kitaifa wa michezo ambao utawekeza  katika kuandaa vipaji vya michezo mbalimbali kuanzia ngazi ya chini ili kuifanya sekta hiyo iwe na tija kwa taifa.

Zaidi ya hayo, Dkt. Abbasi amesema Serikali imefanya maamuzi muhimu ambapo Chuo cha Michezo Malya kinajipanga kuwa na programu ya vijana wenye vipaji vya michezo ili wafundishwe zaidi, pia inaendelea kusajili vituo vya kufundisha michezo vya wadau.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger