Saturday 6 June 2020

Maonesho Ya 44 Kimataifa Ya Biashara Ya Dar Es Salaam (44th DITF) Kuanzia Tarehe 1 – 13 Julai, 2020 Katika Uwanja Wa Maonesho Wa Mwl. J.K. Nyerere

...
Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inapenda kuwataarifu Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Jumuiya za Wafanyabiashara na Wananchi wote kwa ujumla kuwa inaendelea na maandalizi ya Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayotarajiwa kuanza tarehe 1 hadi 13 Julai, 2020 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam. 

Lengo la Maonesho haya ni kutoa fursa ya kutafuta masoko ya mazao na bidhaa za kilimo, viwanda na huduma nchini. Kauli Mbiu ya Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) ni “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” ikilenga kutambua mchango wa Sekta ya Kilimo na Viwanda katika kuzalisha ajira na kujenga biashara endelevu.
 
Uratibu wa Maonesho unazingatia kanuni za Afya kwa lengo la kuhakikisha kuwa Uwanja wa Maonesho unakuwa salama kwa Waoneshaji na Watembeleaji kwa kuchukua hatua zote stahiki za kujikinga na maambukizi ya COVID-19.
 
Ili kuendana na hali halisi na kufikia wigo mkubwa zaidi wa Wazalishaji na Wanunuzi, Mikutano yote ya ana kwa ana ya Wafanyabiashara (B2B) itaandaliwa na kuratibiwa kwa njia ya mtandao. Lengo la Mikutano hii ni kuimarisha upatikanaji wa masoko endelevu ya bidhaa na huduma. 

Aidha, ili kurahisisha utembeleaji wa Maonesho, watembeleaji watapata fursa ya kununua tiketi kupitia simu za mikononi. Vilevile, Watembeleaji kutoka ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kutembelea Maonesho kupitia mtandao (Live streaming and virtual exhibition). Kutakuwa pia Banda Maalumu litakalo tangaza bidhaa za kilimo yakiwemo mazao ya kimkakati.
 
Wizara ya Viwanda na Biashara inatoa wito kwa Wafanyabiashara, Wamiliki wa Viwanda vyote nchini, Wakulima, Taasisi za Umma, Halmashauri za Wilaya na Taasisi Binafsi kushiriki katika Maonesho haya ili kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa za kilimo, viwanda, mifugo, uvuvi na madini zinazozalishwa nchini na kuhamasisha Wananchi kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
 
Imetolewa na;
Innocent L. Bashungwa (Mb.)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger