Serikali iko mbioni kumaliza changamoto za makazi ya Askari nchi nzima ikiwa ni mkakati wa Uongozi wa Awamu ya Tano kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu katika vyombo vilivyopo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji.
Hayo yamesemwa Visiwani Pemba na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni baada ya kukagua nyumba 14 kati ya nyumba 400 zilizopo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji na nyingine zushakamilika huku gharama za ujenzi wa nyumba hizo ni Bilioni 10 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Magufuli, mwezi April, 2018 mkoani Arusha wakati wa Kumbukumbu ya Hayati Abeid Amani Karume.
“Serikali ya Awamu ya Tano imekua inatambua changamoto za makazi ya askari na ujenzi wa nyumba hizo 400 ulishaanza nchi nzima na nyingine zishakamilika, napenda kuwaahidi askari wetu changamoto hiyo ya makazi itakua historia ndani ya muda mfupi, nimetembea baadhi ya mikoa nimeona jinsi askari wetu wanavyoishi.”alisema Masauni
“…lakini baadhi ya mikoa tushajenga nyumba ikiwemo nyumba za askari magereza Ukonga, nyumba za uhamiaji Iyumbu Dodoma, nyumba za polisi Medeli, Dodoma na mikoa yote nchini kuna nyumba ambazo askari wetu washaanza kukaa” aliongeza Masauni
Wakizungumza baadhi ya askari wanaokaa katika nyumba hizo za Pemba waliishukuru serikali kwa kuwajengea makazi ambayo yamepunguza changamoto hiyo huku wakiweka wazi ilikua ngumu kuchanganyika na raia mtaani lakini sasa wanaamini makazi hayo yatawafanya wafanye kazi zao kwa umakini na uadilifu mkubwa.
Mradi huo wa nyumba zilizopo katika eneo la Mfikiwa ChakeChake Kusini Pemba umekamilika na unajumuisha nyumba 14 ambapo jumla ya familia 14 za askari polisi zinatumia makazi hayo.
0 comments:
Post a Comment