Idara ya sera na mipango ya Wizara ya Kilimo imetakiwa kubainisha kiasi gani cha fedha kimewekezwa Kwenye Kilimo kutoka serikalini, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 22 Aprili 2020 wakati akizungumza na watumishi wa idara hiyo katika ukumbi wa Wizara hiyo maarufu kama KILIMO IV Jijini Dodoma.
Amesema kuwa pamoja na majukumu muhimu yanayofanywa na Wizara ya Kilimo lakini idara hiyo inapaswa kuongeza juhudi na weledi katika utendaji kazi wake wa kila siku ili kuongeza Tija na uzalishaji wa mazao ya wakulima.
Waziri Hasunga ameitaka idara hiyo kubainisha Takwimu mbalimbali za uzalishaji wa mazao, bei za mazao, uchambuzi, ikiwa ni pamoja na takwimu za Mazao ya mboga, maua na matunda.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio makubwa ambayo yameonekana katika sekta ya kilimo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli lakini bado sekta ya kilimo inapaswa kuimarishwa zaidi ili kuwa na mafanikio makubwa zaidi katika kilimo.
“Nchi zilizoendelea Duniani zimefanya nini na kwa nini Tanzania tupo nyuma Kwenye kilimo, na Kuna viwanda vingapi vya kuchakata mazao ya Kilimo” Alihoji Mhe Hasunga wakati wa kikao kazi hicho
Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameitaka idara hiyo kubainisha kuhusu Uongezaji thamani upoje na sera inasema nini kuhusu uongezaji thamani wa mazao.
Kadhalika, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameitaka idara ya sera na mipango kubainisha kuwa Sera ya masoko ipoje na wataalamu wanasemaje kuhusu hali ya masoko. Pia ametaka kufahamu hali ikoje kupitia sera ya usalama wa chakula, Sera ya Ushirika, Sera ya matumizi Bora ya ardhi na Tunakwama wapi Kwenye kilimo
MWISHO
0 comments:
Post a Comment