Chuo Kikuu cha Kenyatta
Baadhi ya raia waliowekwa Karantini eneo la Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya, wamezua tafrani baada ya kutishia kujiua kwa kujirusha kutoka ghorofani, wakidai kunyanyaswa na Serikali wakilazimishwa kulipa ada ya Karantini.
Raia hao wamesema hawana uwezo wa kulipa ada hiyo, kwani waliambiwa kuwa Serikali imesimamia kila kitu kuhusu wagonjwa watakaowekwa Karantini.
Kupitia video iliyoripotiwa na kituo cha televisheni cha NTV nchini humo, imewaonesha raia hao wakipiga kelele kuwa wanataka kujirusha kutoka ghorofani kutokana na kadhia hiyo, huku wahudumu wa afya wakiwasihi kuacha kufanya hivyo.
Baada ya kubadilisha uamuzi wao, mmoja wa watu waliotaka kufanya kitendo hicho amesimulia, "nilitolewa nyumbani nikiwa na shida ya kifua na kukohoa, nikapelekwa kupimwa kisha nikaletwa hapa Kenyatta, lakini siku nataka kutoka nikaambiwa huwezi kutoka mpaka ulipe, nikauliza nalipa nini wakati Serikali imesimamia kila kitu?".
Mgonjwa mwingine amesema kuwa aliletwa chuoni hapo akisumbuliwa na kifua na si Corona lakini hakupewa matibabu na amewekwa chuoni hapo kwa siku zaidi ya 21 kwa kuwa hana pesa za kulipa.
Kwa pamoja, wananchi hao wameiomba Serikali ya Kenya kuwaangalia upya kwa kuwa hawana pesa za kulipia, hivyo wanaombwa waachiwe kwa sababu wao si wahalifu.
0 comments:
Post a Comment