Tuesday 28 April 2020

GGML YATOA SH BILIONI 1.6 KUUNGA MKONO MAPAMBANO DHIDI YA CORONA

...

Mmoja wa wakazi wa Mji wa Geita wakiosha mikono kwa maji tiririka na sabuni kutoka kwenye vifaa vilivyotolewa na kampuni ya GGML
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Geita wakiosha mikono kwa maji tiririka na sabuni kutoka kwenye vifaa vilivyotolewa na kampuni ya GGML
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Richard Jordinson akizungumza

***

NA MWANDISHI WETU

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa Sh bilioni 1.6 kuunga mkono juhudi za Serikali kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona ambayo hadi sasa yamesambaa katika nchi 210 duniani Tanzania ikiwemo.

Pia GGML imezindua mikakati kadhaa ya kupambana na janga la virusi hivyo vinavyosababishwa ugonjwa wa Covid–19 katika eneo lake la kazi na kwa jamii zinazozunguka mgodi wake.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Wayne Louw imefafanua kuwa katika fedha hizo, Sh bilioni 1.1 zitaelekezwa kwenye ngazi ya kitaifa kupitia Mfuko Maalum wa mapambano dhidi ya Covid – 19 ambao unasimamiwa na ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema fedha zingine kiasi cha Sh milioni 500 zitatumika kwa ajili ya kusaidia juhudi zinazofanywa katika ngazi ya mkoa na jamii, zitakazojumuisha ununuzi wa vifaa-tiba muhimu na vitendea kazi kama vile vifaa vya kujikinga, barakoa, mashine za kusaidia upumuaji, nk.

Aidha, alisema GGML kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) imeweka matanki 10 ya maji yenye uwezo wa kubeba lita 1000 kila moja kwa ajili ya kuwezesha watu kunawa mikono.

Alisema jukumu la GEUWASA litakuwa ni kujaza maji katika matenki hayoambayo yamewekwa katika maeneo yenye watu wengi mjini Geita.

“GGML pia itatoa dawa aina ya Chlorine ili kutakasa maji hayo, na kwa hiyo hakutakuwa na ulazima wa kutumia sabuni. Matenki mengine yanaendelea kutengenezwa kwa ajili ya Watoto na watu wenye ulemavu.

“Nia yetu ni kuendelea na shughuli zetu kama zilivyopangwa na tunatumaini kwamba janga hili litakwisha hivi karibuni. Kwetu sisi, shughuli zetu zinajumuisha uzalishaji wa dhahabu na pia utekelezaji wa miradi ya kusaidia jamii inayotuzunguka,” alisema.

Naye Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya afya mahali pa kazi, Dk. Kiva Mvungi alisema katika kujenga uelewa juu ya janga hili kwa jamii zinazozunguka mgodi, kampuni hiyo imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye taarifa za virusi ndani na nje ya mgodi.

“Katika kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya uelimishaji juu ya janga la Covid-19, GGML imeingia ubia na Rubondo fm, ambacho ni kituo cha redio kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Chini ya ubia huu, Kampuni ya GGML inagharimia uandaaji wa tangazo, na kituo cha Rubondo fm kitatoa mchango wake kwa kurusha tangazo hilo bila malipo",alisema. 

Alisema Kituo cha Rubondo fm kilianzishwa kwa ufadhili wa GGML chini ya Mpango wa uwajibikaji kwa Jamii (Corporate Social Responsibility) wa kampuni hiyo.

“Tunafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali. Maofisa wetu wawili wameteuliwa na Mkuu wa Mkoa kuwa sehemu ya kamati maalum iliyoteuliwa kupambana na janga hili hapa Geita. Wawakilishi wetu hawa wanahakikisha kwamba mipango yetu ya kupambana na Covid – 19 inaendana na ile ya Serikali”, alisema Dk. Mvungi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger