Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa mara ya pili, imetupilia mbali maombi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ya kujaribu kupinga uamuzi wa kuvuliwa ubunge.
Maombi hayo yalitupwa mwishoni mwa wiki mbele ya Jaji Yose Joseph Mlyambina, baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na jopo la mawakili kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
“Baada ya kusikiliza hoja za mapingamizi na majibu, mahakama inakubaliana na hoja za Serikali na inaona maombi hayana msingi kisheria kwa kuwa sheria hairuhusu rufaa kwa kesi inayofafana na hiyo,”alisema.
Katika maombi hayo namba 42 ya mwaka 2019 ya kutaka ridhaa ya Mahakama Kuu kumruhusu kukata rufaa yaliyofunguliwa Oktoba 10, 2019,Tundu Lissu alikusudia kupinga uamuzi wa yeye kuondolewa ubunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kanuni za Kudumu za Bunge kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao zaidi ya vitatu vya Bunge pasipo ruhusa ya maandishi ya Spika.
Maombi hayo yalipingwa vikali na mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa madai hayakustahili kusikilizwa kwa kuwa yalikinzana na kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Rufani kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Na. 25 ya mwana 2002.
Upande wa Serikali, ulidai Lissu hakuwa na haki kisheria kupinga uamuzi wa Jaji Sirilius Matupa ulitolewa Septemba 9, mwaka jana wa kumnyima ridhaa kufungua shauri la mapitio ya kiutawala uamuzi ambao uliishia kwa yeye kupoteza ubunge.
Ilielezwa na mawakili wa Serikali, uamuzi wa Jaji Matupa haukupaswa kupingwa kwa njia ya rufaa kwa kuwa uamuzi huo haukumaliza shauri kama inavyopaswa kisheria.
Upande wa Serikali uliishawishi mahakama katika kesi mbalimbali, Mahakama iliamua kuwa rufaa haiwezi kukatwa kwa shauri ambalo limeisha katika hatua za awali kama ilivyokuwa kwa kesi ya Lissu ambaye alikuwa akiomba ridhaa ya kuwasilisha maombi ya mapitio na akanyimwa ridhaa kwa kuwa maombi yake hayakuzingatia Sheria.
0 comments:
Post a Comment