Wednesday, 2 October 2019

Maabara Bubu 13 Zafungiwa, Huku 48 Zikipewa Onyo Kali

...
Na Rayson Mwaisemba WAMJW- DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, imezifungia jumla ya maabara 13, ambazo ni sawa na asilimia 21% kati ya Maabara 61 zilizokaguliwa, huku ikitoa onyo kali kwa Maabara 48 kutokana na baadhi ya Maabara hizo kutokidhi viwango vya kutoa huduma za upimaji.

Hayo yamesemwa leo na Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi kutoka Wizara ya Afya Bw. Dominic John Fwiling’afu wakati wa ziara ya ukaguzi wa hali ya utoaji huduma za upimaji katika maabara zilizopo Jiji la Dodoma.

“Tuliweza kufunga Maabara 13, kati ya maabara 61 tulizozikagua, na hizo maabara 13 ni sawa na asilimia 21% ambazo tuliweza kuzifungia, huku Maabara 8 sawa na asilimia 20% ni Maabara zilizo ndani ya vituo vya kutolea huduma kama vile zahanati, na maabara zinazojitegemea ni 5 sawa na asilimia 24%” amesema Bw. Dominic Fwiling’afu

Amesema kuwa Bodi ya Maabara Binafsi katika kutekeleza majukumu yake, inaendeleza mpango wake wa kukagua Maabara Binafsi zote nchini ili kuhakikisha zinatoa huduma kulingana na miongozo ili kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Aliendelea kusema kuwa zoezi hilo limeanza Jijini Dodoma, huku lengo likiwa kukagua jumla ya Maabara 106 ili kujiridhisha utoaji huduma sahihi kwa wananchi, ikiwemo kukagua kama Wataalamu waliopo wanakidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria.

Pia, Bw. Dominic Fwiling’afu amesema kuwa licha ya kukagua ili kujiridhisha na ubora wa huduma zinazotolewa na Maabara hizo, Bodi hiyo inajukumu la kuangalia ulipaji wa tozo mbali mbali uliowekwa kwa mujibu wa Sheria na kujiridhisha kama Maabara hizo zimetimiza masharti wakati wa uanzishwaji wake.

“Sambamba na hiyo Bodi ya Maabara Binafsi inajukumu la kuangalia ulipwaji wa tozo mbali mbali katika uendeshwaji wa Maabara hizo, kama zote zinafuata miongozo kwa mujibu wa Sheria na kuangalia utendaji na utoaji huduma katika Maabara hizo kama ni salama na sahihi” amesema Bw. Dominic Fwiling’afu

Aidha, Bw. Dominic Fwiling’afu ameongeza kuwa, mbali na kuzifungia baadhi ya Maabara hizo ambazo hazijakidhi vigezo kulingana na Sheria na miongozo, Bodi imeendelea kutoa ushauri kwa wamiliki na Wataalamu wa Maabara ili kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Mbali na hayo, Bw. Dominic Fwiling’afu ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapata huduma kwenye Maabara zilizosajiliwa na kutambulika kwa mujibu wa Sheria, huku akiwaagiza Wamiliki wa Maabara binafsi kuhakikisha wanabandika leseni ya usajili wa Maabara hizo katika eneo la mapokezi ili kiweze kuonekana.

Akielezea sababu za kuzifungia baadhi ya Maabara, Mkaguzi kutoka Bodi ya Maabara Binafsi Wizara ya Afya Bi. Mayasa Rico amesema kuwa kukosekana kwa Wataalamu wa Maabara wenye sifa, kuendesha Maabara hizo bila ya kuwa na vibali, kutokuwa na miongozo na kanuni ya Bodi, miundombinu kutokidhi viwango, kutoa huduma za matibabu na kutoa huduma baadhi ya huduma bila kibali.

“Kukosekana kwa Wataalamu wenye sifa, kuendesha Maabara bila kuwa na vibali,kutokuwa na miongozo na kanuni ya Bodi,majengo kutokidhi viwango kulingana na taratibu, kupima vipimo visivyoruhusiwa bila ya vibali na kutoa huduma za matibabu ndani ya Maabara ni baadhi ya sababu zinazopelekea kufungwa kwa Maabara hizo” amesema Bi. Mayasa.

Kwa upande wake, Mkaguzi kutoka Bodi ya Maabara Binafsi Wizara ya Afya Edinanth Ģareba, amedai kuwa jumla ya maabara 42 tu ndio zimesajiliwa na kutambulika kisheria kati ya Maabara 61 zilizo kaguliwa, ambazo ni sawa na asilimia 69%, huku akisisitiza kusajili Maabara hizo jambo litalosaidia kuzifuatilia Maabara hizo kwa ukaribu na kuzisa idia namna bora ya kutoa huduma ya vipimo kwa wananchi.

Aidha, Edinanth Ģareba aliendelea kutoa onyo kali kwa wauguzi na tabibu wanaopima sampuli za wagonjwa, na kusisitiza kuwa shughuli zote za maabara zinapaswa kufanywa na Mtaalamu wa Maabara tu na si vinginevyo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger