KUHUSU WANACHUO WALIOKUWA WANASOMA STASHAHADA MAALUM YA UALIMU KATIKA CHUO KIKUU CHA DODOMA
1.0 UTANGULIZI Itakumbukwa kwamba tarehe 28 Mei, 2016 Serikali iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati Chuo Kikuu Dodoma. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na mgomo wa walimu uliokuwa umedumu kwa takribani wiki 3. Wanafunzi waliosimamishwa masomo walikuwa wamegawanyika katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza lilikuwa ni wanafunzi 6,595 waliodahiliwa katika Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari na kundi la pili lilikuwa na wanafunzi 1,210 waliodahiliwa katika mafunzo ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi. 2.0 SIFA ZA KUJIUNGA NA PROGRAMU MAALUM YA STASHAHADA Baada ya hatua ya kuwaondoa wanafunzi chuoni kuchukuliwa, Serikali ilifanyaUchambuzi wa wanafunzi hao kwa lengo la kujiridhisha na sifa zao. Sifa zilizotakiwa ni ufaulu wa Daraja la I hadi la III na credit mbili au zaidi katika masomo ya Sayansi na Hisabati.Mchanganuo wa ufaulu wa Kidato cha Nne kwa wanafunzi hao ni kama ifuatavyo: Jedwali Na. 1: Mchanganuo wa wanafunzi kwa ufaulu
Jedwali Na. 1 linaonesha kuwa kulikuwa na wanafunzi 52 waliopata Daraja la IV kinyume na matakwa ya Programu ambapo mwanafunzi alitakiwa awe na ufaulu wa Daraja la I – III. Aidha, uchambuzi zaidi ulifanyika kwa wanafunzi wenye ufaulu wa Daraja la I-III ili kujiridhisha kama wamekidhi kigezo cha kuwa na ufaulu katika masomo mawili kwa kiwango cha C-A. 3.0 UCHAMBUZI WA SIFA ZA WANAFUNZI Uchambuzi wa sifa kwa kuzingatia vigezo vya kujiunga vilivyowekwa umebainisha yafuatayo: 1. Wanafunzi 6,595 walidahiliwa kusoma programu ya Stashahada Maalum ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari kwa Masomo ya Hisabati na Sayansi.Kati yao,6305 walikuwa na sifa stahiki ambazo ni ufaulu kwa Daraja la I – III na ufaulu kwa kiwango cha gredi C-A katika masomo mawili ya Sayansi. Wanafunzi 4,720 walikuwa mwaka wa kwanza na wanafunzi 1,585 walikuwa mwaka wa pili. Mchanganuo wa ufaulu wao umeainishwa katika Jedwali Na. 2. Jedwali 2: Ufaulu wa Wanafunziwa Stashahada ya Ualimu Sekondari Waliokidhi Vigezo vya Udahili
2. Wanafunzi 290 hawakuwa na sifa za kudahiliwa kwenye Programu maalum ya ualimu wa Shule za Sekondari. Matokeo ya Kidato cha Nne ni kama ifuatavyo:
Jedwali linaonesha kuwa: a) Wanafunzi 21 walikuwa na ufaulu wa Daraja la IV wakati walipaswa kuwa na Daraja la I - III; b) Wanafunzi 269 walikuwa na ufaulu wa kati ya Daraja la I-III (II – 9; III - 260) lakini hawakuwa na Ufaulu wa kiwango cha C-A kwa masomo mawili ya Sayansi. 3.1 Programu ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi Uchambuzi wa sifa ulifanyika pia kwa wanafunzi 1,210 waliokuwa wamedahiliwa katika Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi na kubaini yafuatayo: (i) Wanafunzi 29 wa mwaka wa II walikuwa ni walimu wa shule za msingi ambao walikuwa wamehitimu Kidato cha Nne na kuhudhuria mafunzo ya Ualimu wa Cheti (Daraja la IIIA) ambao walikuwa na uzoefu kazini wa miaka miwili au zaidi. Mchanganuo wa matokeo yao ya Kidato cha Nne umeainishwa katika jedwali lifuatalo:
(ii) Wanafunzi 1,181 walikuwa ni wahitimu wa Kidato cha Nne ambao mchanganuo wa matokeo yao ya Kidato cha Nne umeainishwa katika Jedwali lifuatalo:
Kufuatia uchambuzi uliofanyika, Serikali imefanya maamuzi yafuatayo: 4.1 Kundi la Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari (i) Kwa kuwa uchambuzi umebainisha kuwa Wanafunzi wenye ufaulu wa Daraja la I na la II ambao pia wamefaulu masomo mawili ya Sayansi kwa kiwango cha C-A ni 382 (mwaka wa I -134 na mwaka wa II - 248), wanafunzi hao ndiyo pekee watakaorudishwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma ili wakamalizie mafunzo yao katika Chuo hicho. (ii) Wanafunzi 4,586 wa mwaka wa I wa Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika Vyuo vya Ualimu vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo yao. (iii) Wanafunzi 1,337 wa Mwaka II watahamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Korogwe na Kasulu kumalizia masomo yao. (iv) Wanafunzi 290 waliokuwa wamedahiliwa kusoma Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari Masomo ya Sayansi na Hisabati ambao hawana sifa stahiki wanashauriwa kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizo nazo kwenye chuo chochote wanachotaka wao. 4.2 Kundi la Programu ya Ualimu wa Elimu ya Msingi Wanafunzi katika kundi hili hawakuwa sehemu ya program maalum ya kupunguza uhaba wa walimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati. Walikuwa wanaandaliwa kufundisha shule za msingi wakati lengo la Programu Maalum ilikuwa ni kukabiliana na tatizo za uhaba wa walimu wa Sekondari. Maudhui ya program waliyokuwa wanasoma hayakuwa sawasawa na yale ya Programu ya Ualimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati. (v) Wanafunzi 29 wa mwaka wa II wenye Cheti cha Daraja IIIA waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Ualimu wa Shule za Msingi watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo yao kwa gharama zao wenyewe. (vi) Wanafunzi 1,181 waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Kawaida ya Ualimu wa Elimu ya Msingi waombe mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo mahali popote watakapotaka wao. 5.0 GHARAMA ZA MASOMO Serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM. Aidha, wanafunzi watakaohamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Serikali watapewa mkopo wa kiasi cha Sh. 600,000/= kwa mwaka ambayo ni ada ya Mafunzo ya Ualimu itakayolipwa moja kwa moja Chuoni. 6.0 HITIMISHO (i) Wanafunzi wote wanaorejeshwa Chuo Kikuu cha Dodoma wataanza masomo mwezi Oktoba 2016. (ii) Wanafunzi watakaohamia katika Vyuo vya Ualimu wataendelea na mafunzo yao mwezi Septemba mwaka 2016. (iii) Wanafunzi wote watatakiwa kuripoti wakiwa na vyeti vyao halisi vya Kidato cha Nne ambavyo vitahakikiwa kabla hawajapokelewa rasmi kwenye vyuo walivyopangiwa. (iv) Majina ya wanafunzi wenye sifa na vyuo walivyopangiwa pamoja na wale wasio na sifa yanapatikana katika tovuti ya Chuo Kikuu cha Dodoma ambayo ni www.udom.ac.tz. IMETOLEWA NA Prof. Joyce Lazaro Ndalichako (Mb) WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA 19 Julai, 2016 |
0 comments:
Post a Comment