Friday 29 July 2016

Asilimia 60 ya waajiriwa hawana mikataba ya kazi

...

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezindua Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara kwa Mwaka 2015 ambacho kimebainisha kuwa asilimia 60 ya wafanyakazi nchini hawana Mikataba stahiki ya kazi, jambo linalosababisha serikali kupoteza mapato ya kodi.
Aidha ripoti imebainisha Mikataba mingine iliyopo kuwa na upungufu mwingi ikiwa ni pamoja na miongoni mwao kuandikwa kwa lugha isiyoeleweka na mingine kuandikwa kwa ufupi na kushindwa kujumuisha mambo ya msingi.
Nalo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), limekiri kuwepo kwa matatizo hayo kwa wafanyakazi lakini likafafanua kuwa wengi ni waoga kufukuzwa kazi, hivyo wanashindwa kujitokeza hadharani na kueleza yanayowasibu.
Akizungumzia ripoti hiyo wakati wa uzinduzi jijini Dar es Salaam jana, Mtafiti wa Taarifa wa LHRC Clarence Kipobota alisema miongoni mwa wafanyakazi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kukosa Mikataba halali ya kazi ni pamoja na waandishi wa habari pamoja na madereva.
Alisema kutokuwepo pia kwa vyama vya wafanyakazi katika maeneo ya kazi, kumekuwa kukichangia wengi wao kukosa makubaliano ya pamoja.
“Hali ya ajira na mahusiano kazini inakabiliwa na changamoto kubwa, wengi hawana Mikataba na matokeo yake Serikali inakosa kodi ambayo ingekatwa katika Mishahara inayofahamika kama PAYEE,” alisema Kipobota huku akiitaka Tucta kusaidia kumalizwa kwa tatizo hilo.
Aidha alisema utatuzi wa masuala ya kazi unaofanywa na Tume ya Usuluhishi wa Migogoro sehemu ya Kazi (CMA) umekuwa hauna kasi kama inavyotakiwa kumalizika ndani ya siku 60 ambapo mashauri mengi huchukua muda mrefu.
Alisema asilimia 57.5 ambayo ni sawa na mashauri 30,095 ndio ambayo yamesikilizwa tangu mwaka 2006 hadi 2015.
Kuhusu suala la ardhi alisema ardhi za vijiji zinaendelea kuchukuliwa ambapo wawekezaji wa ardhi wamekuwa wakichukua eneo kubwa na kuliacha bila kuendelezwa huku wananchi wakiendelea kuhangaika jambo linalozalisha migogoro ya wakulima na wafugaji.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger