Friday 29 July 2016

Mkapa ahimiza sera zinazotekelezeka

...

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinatoa kipaumbele katika uongozi unaojali masuala ya utawala bora, uzalendo na sera zinazotekelezeka ili kuweza kupata maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Mkapa pamoja na marais wengine wastaafu wa nchi za Afrika, endapo nchi hizo zitashindwa kutumia njia sahihi kufikia malengo yake ya maendeleo zitajisababishia kuwa nchi zisizo na usawa katika mgawanyo wa mali na migogoro.
Akizungumza katika Kongamano la Viongozi wa Afrika lililofanyika jijini Dar es Salaam jana, Rais Mkapa alisema ni lazima Waafrika wajitume na kujiletea maendeleo yao wao wenyewe na kusisitiza kuwa hakuna mtu yeyote wa mataifa ya nje atakayewasaidia.
Alisema ni wakati muafaka sasa kwa Waafrika kuungana na kutumia uwezo walionao kuhakikisha ajenda ya Umoja wa Afrika (AU) ya kutafuta na kutumia rasilimali zinazopatikana Afrika ifikapo mwaka 2063 inafanikiwa.
“Kaulimbiu ya mwaka huu, inasema namna Sekta ya Biashara inavyoweza kuleta mageuzi Afrika kwa haraka. Kama mnavyojua katika ajenda yetu ya 2063 tumejiwekea malengo ya kuhakikisha nchi za Afrika zinakua kiuchumi na kuwa na maendeleo endelevu…lakini ili haya tuyafanikishe ni lazima tutegemee zaidi ushiriki wa Waafrika,” alifafanua.
Alitolea mfano kipindi cha uongozi wa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere kwamba aliweka msisitizo katika masuala ya watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora ili kuwapatia maendeleo Watanzania.
“Ardhi tuliyonayo inaweza kutumika kwa manufaa yetu, watu tulionao tunaweza kuwahamasisha kuwajibika, sera nzuri zinaweza kusaidia kusukuma watu kuleta maendeleo lakini pia utawala bora unatengeneza njia kwa maendeleo endelevu,” alisema Mkapa.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Wachimba Madini cha Afrika Kusini na mtoa mada mkuu katika mkutano huo, Sipho Nkosi, alisema Afrika imekuwa na maendeleo mazuri ya kibiashara kwa muda mrefu na kusisitiza kuwa kwa mwenendo uliopo, bara hilo litaleta mageuzi makubwa duniani.
Nkosi ambaye ni bilionea wa tatu kwa utajiri Afrika Kusini, alisema kila nchi ya Afrika ina wajibu kutengeneza mazingira mazuri na fursa kwa wafanyabiashara Waafrika ili kuwajengea uwezo na kuwapa nafasi ya kuwa sehemu ya mafanikio ya nchi yao.
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Msumbiji Joaquim Chissano, alisisitiza umuhimu wa kutafuta mbinu bora za kisasa za kutumia ardhi ili iweze kuleta maendeleo katika nchi hizo za Afrika badala ya kutegemea zaidi mikakati na mbinu za nchi za Magharibi.
Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika, Frannie Leautier, alisema nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na ukosefu wa viongozi wenye mikakati na uwezo wa kuziletea mabadiliko ya kiuchumi hali inayosababisha nchi hizo uchumi wake kukua taratibu.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, alisema viongozi wanaochukia ubinafsi ndio chachu katika kuwawezesha Waafrika kukua kimaendeleo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger