Stori: Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM: Kimenuka!
Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mafahari wawili wa Bongo Fleva, Ali
Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kudaiwa
kutupiana vijembe vya kufa mtu baada ya kuwepo kwa madai ya Kiba
kuhujumiwa.
Kwa mujibu wa chanzo makini, ili kuweka
hujuma ya kibiashara, hivi karibuni, pamoja na kukanusha mara kadhaa
kutokuwa na tatizo na Kiba, Diamond alidaiwa ‘kutengeneza’ kwa makusudi
penzi la mwigizaji Jacqueline Wolper Massawe na msanii wa Wasafi Classic
Baby (WCB), Rajabu Abdulhan ‘Harmonize’ kisha kuvujisha video ya
uhusiano huo mpya siku ambayo Kiba alikuwa akiuachia wimbo wake mpya wa
Aje (Jumamosi iliyopita), lengo likiwa kuhamisha upepo mashabiki kutoka
kwenye wimbo mpya na kujali mapenzi ya wawili hao.
“Ni hujuma ya kibiashara, Diamond na
uongozi wake wameamua kumfanyia Kiba ili wimbo wake ukose kiki kwa
watu,” kilidai chanzo chetu.
VIJEMBE VYATAWALA
Hata hivyo, kwa mujibu wa mmoja wa
mameneja wa Kiba ambaye hakupenda jina lichorwe gazetini, amemtupia
vijembe Diamond kwa kudai licha ya hujuma hizo lakini hawawezi kumgusa
Kiba.
“Wanajisumbua, kizuri huwa kinajiuza
chenyewe na huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono. Wameingiza kiki zao
lakini msimu huu hazifui dafu. Wimbo (Aje) umepokelewa vizuri na una
mafanikio makubwa hadi sasa.
AZUNGUMZIA MKATABA
“Kuonesha kwamba Kiba amekubalika, ndani
ya muda mfupi baada ya wimbo huo kuruka hewani, amelamba mkataba na
kampuni ya kimataifa ya Sonny Music. Sasa hapo ndipo utakapoona Ngoma ya
Kiba imekubalika kiasi gani, hawamuwezi huyu,” alisema meneja huyo.
KEJELI SASA!
Kama hiyo haitoshi, meneja huyo alizidi
kutupa vijembe kwa Diamond kwa kueleza kuwa Kiba ni mkongwe hivyo kamwe
hawezi kulingana naye kimuziki.
“Diamond hamuwezi Kiba, ameanza kuimba
wakati Diamond bado hajawa msanii. Ameshafanya mengi kwenye huu muziki
kuliko huyo Diamond, unakumbuka dili la One 8, Kiba aliungana na mastaa
wakubwa katika project iliyokuwa chini ya msanii mkali duniani, R-Kelly
(Robert Sylvester Kelly), Watanzania wanajua,” alisema meneja huyo.
KIBA HUYU HAPA
Alipoulizwa Kiba kuhusiana na vijembe na
kejeli hizo anazodaiwa kuzitupa kwa mpinzani wake (Diamond), alisema
ishu hiyo isiitwe vijembe badala yake ieleweke kwamba ndiyo ukweli.
“Siyo vijembe wala majungu. Huo uliosikia ndiyo ukweli wenyewe,” alisema Kiba.
TEAM DIAMOND WAJIBU MAPIGO
Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii,
wafuasi wa Diamond waliojipa jina la Team Diamond walicharuka kusikia
msanii wao amehusishwa na hujuma za ‘kumuua’ Kiba kibiashara.
“Hana lolote huyo, Diamond ameshafanya
makubwa sana ndani ya muda mfupi kumzidi yeye ndiyo maana anatapatapa
kwa sababu nani asiyejua kuwa Diamond yupo fasta katika kuona fursa
kuliko Kiba?
“Wolper na Harmonize wapo penzini kwa
matakwa yao na si kwa kumuua Kiba, hana jipya,” aliandika mmoja wa
wafuasi wa Diamond kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram.
DIAMOND ANASEMAJE?
Jitihada za kumpata Diamond ili
azungumzie suala hilo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake ya mkononi
kutopatikana hewani hadi tunakwenda mitamboni lakini meneja wake, Babu
Tale alipoulizwa kuhusu suala hilo, alicharuka:
Risasi Jumamosi: Tale
tuambie, hivi kuna ukweli wowote kwamba Diamond na timu yako mlipanga
kumzima Kiba alipokuwa anatambulisha ngoma yake mpya kwa kutupia video
inayoonesha uhusiano wa Wolper na Harmonize?
Tale: “Siyo kweli. Hilo
swali ni la kipuuzi. Sikiliza, ngoja nikuunganishe na bosi wako ili
asikie unavyoniuliza. Nakata halafu nakupigia.
Hata hivyo, Babu Tale hakufanya hivyo na alipopigiwa tena, simu yake haikupatikana.
WOLPER AFUNGUKA
Gazeti hili halikuishia hapo,
lilimtafuta Wolper ili kujua kama ni kweli ametumika kumfifisha Kiba
kimuziki ambapo alisema si kweli kwani penzi lake na Harmonize limetoka
katika mioyo yao.
“Hakuna kitu kama hicho. Sisi
tumependana wenyewe wala hatujashinikizwa na mtu yeyote kuvujisha penzi
letu eti ili kumfanya fulani afifie! Kama imetokea limevuja wakati ambao
huyo Kiba naye ametoa wimbo itakuwa tu imetokea lakini si kwamba
tumedhamiria,” alisema Wolper huku simu ya Harmonize ikiita bila
kupokelewa.
Ugomvi wa Diamond na Kiba ni wa muda
mrefu ambapo huwa na msimu kwani kuna wakati unachachamaa kama sasa na
kipindi kingine unapoa na hakuna anayejua hatima yao.
0 comments:
Post a Comment