Tuesday 24 May 2016

TFDA MWANZA YATOA TAHADHARI JUU YA SUKARI YA "KK"

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Meneja kanda ya ziwa mr Moses.Mbambe

 
 
Na. Mwandishi Wetu
 
Wakati serikali ikiendelea kukabiliana na changamoto ya uhaba wa bidhaa ya sukari na ongezeko la bei ya bidhaa hiyo, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Ofisi ya Kanda ya Ziwa imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya matumizi ya sukari ya Kijiko Kimoja (KK).
 
Sukari ya Kijiko Kimoja inatengenezwa na kiwanda cha 21st Century Food & Packaging Ltd kilichoko Dar es Salaam. Sukari hii ni nyeupe na imetengenezwa kwa kutumia miwa kwa silimia 99.5 na asilimia 0.5 ya vikolezo vingine nyongeza vya utamu.
 
Akiongea na wajasiliamali wa jijini Mwanza katika Semina ya Elimu kwa Umma iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Mwanza, Mkaguzi Mwandamizi wa Chakula wa TFDA Kanda ya Ziwa Julius Panga alisema kuwa kumekuwa na taarifa juu ya baadhi ya watumiaji wakikiuka maelekezo ya matumizi na wafanyabiashara kuuza sukari hiyo kinyume na taratabu.
 
Panga alisema kuwa sukari ya Kijiko Kimoja ni tamu kuliko sukari nyingine kwa kuwa kijiko kimoja ni sawa na vijiko viwili na kuwa kutokana na hali hiyo wazalishaji wameweka taarifa juu ya kifungashio ambazo zinatoa maelekezo juu ya namna ya kutumia bidhaa hiyo.
 
“Sukari hii ina kiwanngo cha juu cha utamu tofauti na sukari nyingine ambazo zinatumika nchini. Hali ambayo imepelekea wagonjwa wa kisukari, wanawake wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kutoruhusiwa kuitumia” alisema Panga.
 
Panga aliongeza kuwa kutokana na upungu wa bidhaa ya sukari nchini baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiiondoa sukari hii katika vifungashio vyake na kuuzwa rejareja hali ambayo ni hatari kwa mtumiaji kwani anakuwa hapati taarifa zilizoko katika kifungashio. “Watengenezaji wa sukari hii wameifungasha katika vifungashio vya kilo moja na nusu kilo. Juu ya vifungashio kuna taarifa muhimu ambazo mteja anapaswa kuzisoma kabla hujatumia. Wauzaji wanapotoa sukari katika vifungashio vyake wanamnyima mteja haki ya kupata taarifa na kufanya uamuzi. Vitendo hivi vimekuwa vikiripotiwa katika maeneo mbali mbali ya kanda ya ziwa”.
 
Pia Panga alisema kuwa wauzaji wa chai katika baadhi ya migahawa wamekuwa wakitumia sukari ya kijiko kimoja  hali ambayo ni hatari kwa afya ya wateja kutoka katika makundi yaliyoanishwa juu ya kifungashio “ Ndani ya migahawa wanaingia watu wote hata wale ambao hawaruhusiwi kutumia sukari hii. Si vizuri kutumia sukari hii katika maeneo haya. Tunashauri wafanyabiashara wa migahawa kutumia sukari nyingine ambayo inaruhusiwa kwa makundi yote” alisema.
 
Maria Paskari ni mkazi wa Kirumba jijini Mwanza, yeye anakili kutumia sukari ambayo ilikuwa tamu kuliko sukari nyingine ambayo amekuwa akitumia. “ Nilimuagiza mtoto kwenda kununua sukari robo dukani. Alileta sukari nyeupe ambayo ilikuwa ni tamu tofauti na ambayo nilikuwa nimeizoea” alisema.
Maria anasema kuwa hakuwahi kusoma maelezo yaliyokuwa katika kifungashio.
“Sijawahi kuona sukari hii ikiwa katika vifungashio vyake. Lakini na mshukuru Mungu mimi sio mjamzito na watoto hawakuitumia. Niliitumia mwenye kwa kuweka kwenye uji ambao watoto hawakuunywa” alisema
 
Kwa upande wake muuzaji wa duka la ‘Mke Mwema’ ililiko Igombe nje kidogo ya jiji la Mwanza Bw. Justin Ntahorija alisema kuwa hajawahi kuuza sukari hiyo lakini baadhi ya wateja wamekuwa wakiwatuma watoto sukari wakiwapa maelekezo kuwa wasinunue sukari nyeupe. “Juzi alikuja mtoto akitaka sukari lakini akanieleza kuwa ameagizwa asinunue sukari kama iliyokuwa kwenye kifungashio alichokuwa amekishika. Nilivyoangalia kifungashio nikakuta ni kile cha sukari ya kijiko kimoja” alisema.
 
Bw Ntahorija aliongeza kuwa katika maeneo ya Igombe kuna taarifa nyingi za kukanganya kuhusu sukari. “Zipo taarifa zinazagaa kuwa sukari nyeupe si nzuri kwa matumizi ya binadamu na atakayekutwa nayo anakamatwa.”alisema.
 
Hata hivyo Panga alisema kuwa Sukari ya Kijiko Kimoja imesajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kama zilivyo bidhaa nyingine za sukari na hivyo kufaa kwa matumizi. “Wananchi hawapaswi kuogopa kununua na kutumia sukari ya Kijiko Kimoja na sukari nyingine nyeupe. Wanachopaswa kufanya ni kufuata maelekezo yaliyoko juu ya kifungashio. Pia wafanyabiashara wanao wajibu wa kuwalinda wateja wao kwa kuhakikisha wanawapatia bidhaa zinazofaa”alisema Panga huku akitoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kusoma taarifa juu ya vifungashio.
 
 



"God who created you without you, will not save you without you" St. Augustine of Hippo (354-430)
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger