Tuesday 31 May 2016

Wabunge wa Upinzani wametoka nje ya bunge kuonyesha kutokuwa na imani na Naibu Spika Tulia Ackson

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Wabunge wa vyama vya upinzani leo wametoka nje kwa mara nyingine kupinga Naibu Spika Dk. Tulia Ackson kuendesha vikao vya Bunge na kumwachia Bunge yeye na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa kutoka Bungeni zinaeleza kuwa, wabunge wote wa upinzani wametoka nje kususia kikao cha Bunge ikiwa ni kutekeleza azimio lao la kutokuwa na imani na Dk Tulia.

Baada tu ya kusomwa dua ya kufungua Bunge asubuhi wabunge hao wametoka nje na kumwacha Dk. Tulia akiwa na wabunge wa CCM pekee.

Hata hivyo Dk. Tulia ameanza kupaniwa na wapinzani tangu jana. Ni kwa madai kuwa wapinzani hawamwamini tena.

Wameeleza kuwa, namna anavyoliongoza Bunge, kauli zake na kuyumba kwake katika kusimamia haki kwa wabunge wa Ukawa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumechochea kuonekana kuwa, nafasi aliyonayo haimstahili.

Kutokana na hali hiyo, Freeman Mbowe ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana aliahidi kuanzisha mgomo dhidi ya Dk. Tulia.

Mbowe aliwaambia hayo wabunge wenzake mjini Dodoma kwenye kikao cha dharura alichoitisha na kushirikisha waandishi wa habari.

Alisema, Dk. Tulia ndio tatizo kuu la Bunge la Kumi na Moja na kwamba, kiongozi huyo wa Bunge kila anapokuwa kwenye kiti na kuongoza Bunge, mtafaruku hutokea.

“Nitapendekeza kuwa kila kikao cha Bunge kinachoongozwa na Tulia Ackson, sote tutoke nje ili kuonesha kwamba hatuna imani naye katika kuendesha shuguli za bunge,” Mbowe alisema jana.

Utekelezwaji wa kauli ya Mbowe umeanza leo ambapo sasa Dk. Tulia amebaki na wabunge wa CCM pekee.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger