Monday 4 December 2023

WIZARA YA AFYA YAJIDHATITI KUTOA HUDUMA BORA KWA WAHANGA WA MAFUTIKO

...

Na Mwandishi wetu,Manyara.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Afya mapema leo Disemba 4, 2023 wamewasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kuona hali ya utoaji huduma na kutoa pole kwa majeruhi 11 wa maafa ya mafuriko yaliyotokea katika mji wa Katesh Wilaya ya Hanang Mkoa wa Manyara ambao wamelazwa katika Hospitali hiyo.

Dkt. Mollel amesema kuwa Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha wanatoa huduma bora za matibabu ili kuokoa maisha ya watu, amesema kuwa hadi sasa Hospitali zote ndani ya Mkoa wa Manyara zimepokea na kuhudumia majeruhi 93 na wote wanaendelea vyema na matibabu.

Dkt. Mollel amesema kuwa Wizara ya Afya imeratibu upatikanaji wa timu za Madaktari kwa ajili ya kuongezea nguvu katika Hospitali za Mkoa wa Manyara ili kuweza kutoa huduma bora na kwa haraka zaidi kwa majeruhi ambapo amebainisha kuwa madaktari hao wametoka katika Mikoa ya Arusha, Dodoma na Singida.

“Huduma zinatolewa vizuri, hakuna kilichokosekana na wagonjwa wanaendela vyema na matibabu, kila kitu kinaenda vizuri kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza jana". Amesema Dkt. Mollel.

Mapema leo asubuhi Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sengida amesema kuwa idadi ya vifo vya watu waliofariki dunia kutokana na mafuriko yaliyotokea imeongezeka kutoka watu 47 hadi kufikia 49 baada ya kupatikana kwa miili mingine miwili.

Hapo baadae Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kufika katika Mkoa wa Manyara kujionea hali ya maafa, kutembelea na kutoa pole kwa majeruhi pamoja na kufanya kikao na watendaji katika kushughulikia maafa ya Katesh.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger