Wednesday 27 December 2023

3,182 KG ZA DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROIN NA METHAMPHETAMINE ZAKAMATWA NCHINI

...

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini( DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya Kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine katika operesheni maalum iliyofanyika Jijini Dar es Salaam na Iringa.

Katika Operesheni hiyo ambayo imefanyika Disemba 5 hadi 23,2023, jumla ya watu saba wamekamatwa kuhusika na dawa hizo ambapo wawili kati yao wana asili ya Asia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 27,2023 Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Aretas Lyimo amesema kiasi hicho cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya methamphetamine na kilogramu 1001.71 aina ya heroin zilizokamatwa katika wilaya ya Kigamboni, Ubungo na Kinondoni Jijini Dar es Salaam pamoja na Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.

Aidha amesema kuwa aina ya dawa ambazo wamezikamata zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za kahawa na majani ya chai.

“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani”. Amesema

Amesema kuwa kiasi cha dawa zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingewza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi”. Amesema

Pamoja na hayo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwani mafanikio haya yametokana na ushirikiano unaotokana na wananchi wanaotoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na weledi na uzalendo mkubwa wa maafisa wa Mamlaka katika udhibiti wa bishara ya dawa za kulevya.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger