Friday 29 December 2023

ADC YAJIWEKA MGUU SAWA UCHAGUZI WA 2024/2025

...

Na Oscar Assenga,TANGA

CHAMA cha Alliance For Democratic Change (ADC-Dira ya Mabadiliko ) kimeanza kujiweka sawa kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na ule Mkuu mwaka 2025 baada ya kutangaza kufanyika kwa uchaguzi wa ndani wa chama hicho kwa mwaka 2024.

Akizungumza leo Katibu Mkuu wa ADC Taifa Doyo Hassan Doyo (Pichani kulia) alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho toleo la tatu la mwaka 2019,Uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hufanyika kila baada ya miakaa mitano.

Alisema kwamba tamko hilo linaonyeshwa katika katiba yao kwenye sura ya nane ibara ya 53(i) “Ukomo wa uongozi ni miaka mitano” na sasa ni wakati wa kufanyika chaguzi ambazo zitawapa fursa ya kupatikana viongozi wapya katika ngazi mbalimbali.

Katibu huyo alisema kutokana na chama kufanya uchaguzi ndani ya chama mnamo mwaka 2019 ambapo ulifanyika Mkutano mkuu mwezi Aprili katika ukumbi wa Hotel ya Madinat Bahri iliyopo Zanzibar.

Aidha alisema kwamba mwaka 2024 viongozi waliopo madarakani wanatimiza miaka mitano tangu kufanyika uchaguzi na mkutano mkuu husika kwa madhumuni ya kuchagua viongozi ambao wako madarakani hadi muda huu.

“Kwa kuzingatia utekelezaji wa miongozo kutoka katika katiba yetu Ofisi ya chama makao makuu inatoa ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho kwa mwaka 2024”Alisema Katibu huyo.

Katibu huyo alisema kwamba uchaguzi huo ngazi ya Tawi utaanza Januari Mosi hadi Januari 31 mwakani wakati ule wa kata utafanyika kati ya Februari Mosi hadi February 29 mwaka 2024 utakaokwenda sambamba na ule wa majimbo.

Alisema baada ya hapo kutafanyika chaguzi ngazi ya wilaya utaanza Machi 1 mpaka Machi 31 mwakani utakaoambatana na ule ngazi ya Kanda huku akiwataka wanachama kuchangamkoa fursa za kuwania nafasi mbalimbali.

Katibu huyo alisema baada ya hapo kutafanyika uchaguzi Mkuu wa chama chicho ambao unatarajiwa kwisha mwezi Mei mwakani na hatimaye kuweza kupata safu mpya za uongozi.

Hata hivyo Katibu huyo alitoa agizo kwa viongozi wote wa chama hicho nchi nzima kusimamia zoezi hilo kwa ufanisi na kushirikisha wanachama wote wa ADC ili kukamilisha chaguzi hizo kwa mafanikio.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger