Wednesday, 1 February 2023

TFS HAIJAZUIA VIBALI VYA KUKAMILISHA MIRADI YA KIMKAKATI YA KUPELEKA UMEME VIJIJINI- NAIBU WAZIRI MASANJA

...
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji wa umeme vijijini Bungeni jijini Dodoma leo.

***************************

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) haijazuia vibali vya kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini kwa kupitisha nguzo za umeme katika Hifadhi za Misitu nchini.

Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji wa umeme vijijini.

“Sheria ya Misitu Sura ya 323 haijazuia upitishaji wa nguzo za umeme katika Hifadhi za Misitu hapa nchini” amesisitiza Mhe. Masanja.

Amefafanua kuwa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002, kimeweka utaratibu kwa taasisi/mtu anayetaka kufanya shughuli mbalimbali ndani ya Hifadhi ya Msitu na utaratibu huo unamtaka mtu huyo au taasisi kuwa na kibali kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kinachomruhusu kufanya shughuli husika.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali kupitia TFS kwa nyakati tofauti imekuwa ikizishirikisha Wizara za kisekta kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini bila kuchelewa.

Katika hatua nyingine, akijibu swali Mbunge wa Mlimba, Mhe. Godwin Kunambi kuhusu utatuzi wa mgogoro kati ya wananchi na vijiji vya Utengule, Iduindembo, Upinde na Tanganyika na Kampuni ya Uwindaji ya Kilombero North’s Limited katika Jimbo la Mlimba amesema Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri nane imeshalitembelea eneo lenye mgogoro kwa lengo la kufanya tathmini na kubaini maeneo halisi yanayostahili kuhifadhiwa kwa maslahi mapana ya Taifa na maeneo mengine wataachiwa wananchi ili waendelee kufanya shughuli zao ikiwemo kilimo, makazi na ufugaji.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger