Tuesday, 14 February 2023

TCDC YAWAKARIBISHA WADAU SEKTA YA USHIRIKA KUJADILI NA KUWEKA MKAKATI WA KUIMARISHA SEKTA YA USHIRIKA NCHINI

...

 

Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) wameandaa mkutano maalum wa wadau wa sekta ya ushirika unaotarajiwa kufanyika Februari 27, 2023, katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Benki ya CRDB.


Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Abdumajid Nsekela katika mkutano na waandishi wahabari uliofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa TCDC, TFC, pamoja na wadau wengine wa sekta ya ushirika.

Nsekela amesema mkutano huo unalenga kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya ushirika ili kujadili maendeleo ya ushirika na kuweka mkakati wa kuimarisha sekta ya ushirika nchini. Nsekela alitoa rai kwa wadau wote wa sekta ya ushirika kuitikia wito wa kushiriki mkutano huo kwani mawazo yao ni muhimu katika kuboresha mfumo wa ushirika.
“TCDC imedhamiria kuuboresha mfumo wa ushirika kuwa wa kibiashara na wa kisasa zaidi ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta mbalimbali, na kuongeza mchango wa sekta hii katika kupambana na umasikini, pamoja na kukuza uchumi wa nchi,” alibainisha Nsekela.

Aliongezea kuwa Kamisheni inaweka nguvu katika uanzishwaji wa mfumo wa kidijitali kuongeza ufanisi kwa Vyama vya Ushirika, kuimarisha Taasisi zinazohusika na usimamizi, kutoa elimu juu ya dhana ya ushirika ili kuongeza ushiriki wa sekta mbalimbali zaidi ya kilimo, na kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika.

“…pamoja na hayo katika mkutano huu tutakwenda pia kujadili Mifumo ya Masoko; usimamizi na matumizi ya mali za vyama, vyama kujiendesha kibiashara, mitaji kwenye vyama vya ushirika; Taswira ya Ushirika kwenye jamii. Maazimio yatakayofikiwa kupitia Mkutano huo yatapaswa kutekelezwa ipasavyo na kila mdau,” alisisitiza.

Nsekela ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TCDC miezi michache iliyopita ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini Mhe. Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan kwa miongozo na jitihada kubwa zinazofanyikwa kuimarisha ushirika, na kuahidi kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo katika kufanikisha malengo waliyojiwekea.

Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mkurugenzi Mtendaji wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege alisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na uboreshaji mkubwa wa sekta ya ushirika ambapo kumepelekea kuongezeka kwa wigo wa ushirika kwenye sekta mbalimbali, kuongezeka kwa mitaji katika vyama, na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali hususan kwatika sekta ya kilimo ambapo tozo za mazao 12 zinakusanywa kupitia ushirika.

Kwa mwaka 2021/2022 Serikali ilipokea jumla ya Shilingi 15,144,077,319.16 zikiwa ni fedha za ushuru unaotokana na zao la korosho uliolipwa na vyama vya TANECU, MAMCU, RUNALI, LINDI MWAMBAO, TAMCU na CORECU. Vilevile, jumla ya Shilingi 1,041,957,051.00 zimepokelewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ushuru kutoka katika Vyama vya Ushirika vya KDCU na KCU kupitia zao la kahawa.
“Katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2022 tumeshuhudia wananchama wa ushirika wakiongezeka kutoka milioni 2.4 hadi milioni 7, lakini pia kumekuwa na uwezeshaji mkubwa wa masoko kupitia mfumo wa ushirika, bila kusahau ongezeko la viwanda vya ushirika ambavyo vimekuwa vikisaidia kuongeza thamani kwa upande wa mazao,” aliongezea.

Dkt. Ndiege alisema pamoja na mafanikio hayo bado kazi kubwa inahitajika kufanyika ili kuufanya ushirika kuwa na tija zaidi katika maendeleo ya wananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Hivyo basi, aliwataka wadau wote wanaohusika na sekta ya ushrika kuhudhuria mkutano huo utakaofanyika Februari 27, 2023.

Baadhi ya wadau wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo ni pamoja na Vyama Vikuu vya Ushirika, Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger