Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima James Mdee amesema, yeye pamoja na wenzake 18 hawatoondoka ndani ya chama hicho na wanaendelea na utaratibu wa kukata rufaa kupinga kufukuzwa.
Mdee amesema hayo leo Jumanne tarehe 1 Desemba 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kutoa msimamo wao baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema.
Mdee na wenzake 18 walituhumiwa kwa “usaliti, kughushi na uasi” wa chama hicho kwa kujipeleka kuapishwa tarehe 24 Novemba 2020 na Spika Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, wakijua chama hicho, hakijapendekeza majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Uamuzi wa kamati kuu, ulitolewa mbele ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe tarehe 27 Novemba 2020 akisema, Mdee na wenzake wamekisaliti chama na kama hawaridhiki na uamuzi huo, wanaweza kukata rufaa baraza kuu ndani ya siku 30 au kuomba radhi.
“Nimejitokeza hapa kuja kutuliza haya mambo maana yanaonekana ni makubwa ila nimekuja kuyaweka yanavyotakiwa yawe, mimi na wenzangu tumekuja hapa kuzungumza nanyi, na niwaambie sisi ni CHADEMA kindakindaki,” amesema Mdee
Kuhusu tuhuma za kununuliwa, Mdee amesema hajawahi kuwaza kununuliwa na wala hatarajii kwani yeye ni miongoni mwa wabunge waliokuwa wanapinga rushwa ndani ya bunge.
“Kumekuwa na maneno mengi, kuna watu wanasema Halima nimenunuliwa, naomba niseme mimi sijanunuliwa, sinunuliwi na sitarajii kununuliwa.”
Pia amezungumzia madai ya wao kugomea wito wa kamati kuu kama mwenyekiti wa chama hicho alivyosema wakati wa kutoa maamuzi ya kamati hiyo, Mdee amesema waliiandikia barua kuomba wapewe muda ili waweze kwenda wakiwa na majibu ya busara.
“Hatukudharau kikao, tuliomba tu Wiki moja mbele, Mbowe amenijenga Mimi, ametujenga, inawezekana kuna Vijana wana ya kwao lakini kuna Viongozi tunawaheshimu sana kwasababu wana mchango mkubwa wa sisi kuwa hapa, lakini hatimaye tumevuliwa Uanachama
“Sisi tumefukuzwa ila tutakuwa Wanachama wa hiyari, ndio maana tumevaa gwanda za CHADEMA, mamlaka za rufaa zipo Baraza Kuu, jana jioni tumepata barua ya taarifa ya uamuzi, mchakato wetu wa rufaa tutaanza kuutafakari ili tuangalie namna ya kutatua tatizo
“Tunaipenda CHADEMA, tunaiheshimu CHADEMA, hatutoondoka CHADEMA, tutabaki Wanachama wa hiyari mpaka tutakapomaliza mchakato wa ndani ya Chama wa kumaliza matatizo yetu, naamini tutayajenga ndani kwetu, leo sizungumzi nje na kuongeza matatizo
“Tuna dhamira za kuchukua hatua za Kikatiba ndani ya Chama chetu na hatua nyingine kwa kadri ambavyo tutaona zina afya kwa pande zote mbili, na kwakweli nimetukanwa sana na hili limenisadia kujua Marafiki wa kweli na wale ambao walikuwa wananisikilizia” -Amesema Halima Mdee
0 comments:
Post a Comment