Saturday, 22 December 2018

WIZARA YA ELIMU YAPIGA MAARUFUKU KUSAMBAZA NYARAKA ZA SERIKALI KATIKA MITANDAO YA KIJAMII

...

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akizungumza na washiriki wa Wizara hiyo (hawapo Pichani) waliohudhuria mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu ambayo yamekamilika leo mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo ya siku tano ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu ambayo yamefungwa leo mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu.

.............................

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha amesema ni kosa kusambaza nyaraka za serikali katika mitandao ya kijamii bila idhini ya Mamlaka husika, hivyo ameagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu na za kisheria kwa watumishi watakaobainika kusambaza nyaraka hizo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati akifunga semina ya mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa baadhi ya Maafisa wa Wizara hiyo na kusisitiza kuwa hakuna mtumishi yeyote wa serikali asiyefahamu kuwa kutoa nyaraka za serikali bila idhini ni kosa la jinai.

“Kumekuwa na usambazaji wa nyaraka za serikali katika mitandao ya kijamii bila idhini na kwa bahati mbaya wakati mwingine unakuta nyaraka imewekwa mhuri wa siri lakini bado unaikuta huko, watumishi wa serikali lazima watambue kuwa kuna utaratibu wa kutoa nyaraka za serikali na kuna sheria ambazo zinawabana wale wote wanaotoa taarifa hizo bila kuidhinishwa”alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Mhe. Ole Nasha amewataka watumishi hao kutambua kuwa hakuna taasisi yeyote inayoweza kufanya kazi bila kuwa na kumbukumbu au nyaraka hivyo amewataka kuhakiksha utunzaji mzuri na salama wa nyaraka hizo kwani ni nguzo muhimu katika kufanikisha utendaji wa majukumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali watu, Moshi Kabengwe amesema mafunzo hayo yametolewa ili kusaidia watumishi kufanya kazi ambazo zitaleta tija kwa jamii inayohudumiwa na kuondoa changamoto ambazo zimebainika katika utoaji wa huduma.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tano na yameshirikisha watumishi zaidi ya 50 kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Makao Makuu, Vyuo vya Ualimu vilivyopo Morogoro na baadhi ya watumishi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger