Thursday, 27 December 2018

VIGOGO MABASI YA MWENDOKASI WAACHIWA KWA DHAMANA , BAADA YA KUKAA MAHABUSU KWA SIKU 60

...
Wafanyakazi saba wa Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART), akiwamo kigogo wa idara ya fedha, wanaodaiwa kuhusika katika mtandao wa uhujumu wa mapato ya mabasi ya mwendokasi kwa kuchapisha tiketi feki kwa abiria wameachiwa kwa dhamana.

Hatua hiyo imekuja baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya siku 60 na Jeshi la Polisi huku wakiendelea kusubiri uamuzi wa jalada lao ambalo lipo kwa mwanasheria mkuu wa Serikali, likisubiri hatima yao kama kufikishwa mahakama ama laa.

Pamoja na kuachiwa, wafanyakazi hao ambao awali walikuwa wanane wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi mara kwa mara huku upelelezi wa kesi yao ukiendelea.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jana alisema tuhuma zinazowakabili wafanyakazi hao ni za kughushi na kuhujumu mapato ya mradi wa mabasi ya mwendokasi, hivyo upelelezi wake unachukua muda mrefu ili kuhakikisha wanapata mtandao mzima.

Alisema awali Jeshi la Polisi lilikuwa linawashikilia wafanyakazi wanane, lakini upelelezi ulipokuwa unaendelea, walilazimika kuwaongeza wafanyakazi wengine watatu.


“Tumelazimika kuwaachia kwa dhamana kwa sababu upelelezi wa kesi yao bado unaendelea, awali walikuwa wafanyakazi wanne, lakini tumelazimika kuongeza wengine watatu na kufikia saba,” alisema.

Mambosasa alisema jalada la watuhumiwa hao lipo mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili aweze kulikagua na kuangalia taratibu za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikishwa mahakamani.

Alisema upelelezi umechukua muda mrefu kutokana na tuhuma za kughushi zinazowakabili ambazo zimehusisha mtandao wa kihalifu.

Mambosasa alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuwakamata na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kihalifu pamoja na kwenda kinyume na sheria za nchi.

Wafanyakazi wanane wa Udart walikaa mahabusu zaidi ya miezi miwili baada ya kukamatwa wakidaiwa wanajihusisha na mtandao wa tiketi za kughushi huku wengine 18 wakiachiwa kwa dhamana.

Awali, Kamanda Mambosasa alidai kuwa watuhumiwa hao wamefanya kosa la kuhujumu mradi wa Serikali ambao ni wa kitaifa na kimataifa kwa kutaka kufifisha jitihada za Serikali.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger