Rais John Magufuli ametaka askari wa Jeshi la Polisi kutoshtakiwa kutokana na makosa yanayojitokeza wakati wakitekeleza majukumu yao ikiwamo kutuhumiwa kuua wahalifu.
Akizungumza jana wakati wa sherehe za kufunga mafunzo kwa askari wa jeshi hilo katika Chuo cha Taaluma za Polisi, Kurasini jijini hapa, Rais Magufuli huku akiahidi kuwa nao bega kwa bega alisema askari wanafanya kazi kubwa ya kuimarisha usalama wa nchi.
Alisema wakati mwingine askari wamekuwa wakishtakiwa kutokana na makosa ambayo hawajayafanya wakati wakitekeleza majukumu yao ikiwamo kutuhumiwa kuua wahalifu na kwamba kufanya hivyo ni kuwavunja nguvu wale wanaojitoa kwa ajili ya Taifa.
“Nataka Jeshi la Polisi linalochukua hatua sio askari anaenda anachukua hatua anashtukia amewekwa ndani, askari amekwenda kupambana na jambazi bahati mbaya jambazi likijipiga lenyewe risasi likafa kule unakuja unamshika askari, hapana,” alisema.
Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alisema askari wa namna hiyo wamejitoa muhanga kulinda amani ya nchi hivyo ni lazima waongezewe vyeo ili kutoa motisha kwa wengine kujitoa kwa ajili ya Taifa lao.
Katika mahafali hayo, jumla ya askari 513 walihitimu kozi za mofisa na wakaguzi wasaidizi wa Polisi baada ya kumaliza mafunzo ya miezi sita huku Mkuu wa chuo hicho, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Anthony Rutta akisema watatu walifariki dunia wakiwa mafunzoni.
0 comments:
Post a Comment