Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Ramadhan Mkalu anayekabiliwa na kesi ya mauaji ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kukamilisha upelelezi wa kesi inayomkabili.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 27, 2018 katika mahakama hiyo baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Mshtakiwa huyo alinyoosha mkono mahakamani hapo na kuomba upelelezi kukamilika mapema.
Wakili wa Serikali, Neema Mbwana amedai mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Janeth Mtega kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine.
"Naomba uelewe kuwa upelelezi unafanywa na polisi hivyo sisi tunasubiri amalize ili tuweze kutenda haki," amedai wakili huyo.
Kufuatia maelezo hayo hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 8, 2019 itakapotajwa tena.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mlaku anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 30, 2017 eneo la Upanga, Makao Makuu ya JWTZ.
Mlaku ambaye ni mwanajeshi wa jeshi hilo katika kambi iliyopo Makongo anadaiwa kumuua mwanajeshi wenzake namba MT 79512, Sajenti Saimon Munyama.
0 comments:
Post a Comment