Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imezuia Makontena zaidi ya 1000 Bandarini, ambayo yanaonekana kuwa ni ya baadhi ya vigogo na makampuni makubwna na endapo hayatolipiwa ndani ya siku 30, yatapigwa mnada.
Baadhi ya taasisi hizo ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Inspekta Jenerali wa Polisi, Klabu ya Simba ya Dar es salaam na kampuni ya Kidoti, inayomilikiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.
Kupitia tangazo la Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Usaje Asubisye, kwenye gazeti la serikali la Daily News la Disemba 19, limeorodhesha mali na wamiliki wake huku likitoa siku 30 kuziondoa.
“Mamlaka ya Mapato inautangazia Umma kuwa bidhaa zilizoorodheshwa zitatambuliwa kuwa zimetelekezwa endapo hazitaondolewa kwenye maeneo ya forodha ndani ya siku 30”, limesema tangazo hilo.
Kampuni ya Kidoti inayojishughulisha na urembo, iliagiza kontena namba HJCU2320135 la nywele bandia (hair weaves) ambazo zimekwama bandarini hapo.
Kukwama kwa makontena hayo bandarini kumekuja ikiwa ni miezi mitatu tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kukumbana na mkasa kama huo baada ya kuagiza makontena 20 yenye samani aliyodai yalikuwa kwa ajili ya shule za mkoa wake.
Makonda alitakiwa kulipa ushuru wa shilingi bilioni 1.2, jambo ambalo lilikuwa gumu kutekelezeka na baadaye TRA ililazimika kuzigawa samani hizo baada ya minada takribani mitatu kukosa wateja.
0 comments:
Post a Comment