Wilaya ya Nyang’hwale imesema itaanza kupima vinasaba kati ya mtoto na mwanamume aliyemuoa mwanafunzi ili kubaini kama ndiye baba halisi.
Hatua hiyo imekuja kutokana na wanafunzi wanaoacha shule kwa kupata ujauzito kukataa kuwataja wanaowapa mimba kwa madai hawawafahamu, lakini baada ya kujifungua huolewa na kudai aliyeoa si baba wa mtoto.
Akizungumza hivi karibuni kuhusu hatua zilizochukuliwa kutokana na wilaya hiyo kurekodi mimba zaidi ya 160 za wanafunzi kwa kipindi cha miaka mitatu, Mkuu wa Wilaya hiyo, Hamimu Gwiyama alisema Serikali imeamua kuwasaka hata ambao wameolewa ili kubaini kama wanaume hao ndiyo waliokatisha ndoto zao za masomo.
“Wanafunzi wengi waliopata mimba sasa wameolewa, lakini wanapohojiwa kujua aliyewapa mimba, wanadai hawamjui au hawamkumbuki, sasa polisi watafanya uchunguzi na kuwahoji wote wawili kujua ukweli itakapokuwa ngumu tutawapima vinasaba.”
Alisema Waraka wa Elimu namba tano wa mwaka 2011 unaoruhusu mwanafunzi kufukuzwa shule baada ya kuwa mtoro kwa siku 90, umechangia wazazi wengi kuwakatisha masomo wanafunzi na kuwaoza.
“Tumeanza operesheni ya kuwasaka wote walioacha shule haijalishi ni baada ya miaka mingapi, bali wote walioacha shule tutawachukulia hatua. Lengo la operesheni hii ni kumaliza tatizo la mimba, tuwajengee hofu wanaume wanaowaoa wanafunzi,” alisema Gwiyama.
Alisema moja ya sababu zinazochangia wanafunzi kubeba mimba ni mila ya Kisukuma ambayo huwapa chumba maalumu cha nje watoto wa kike baada ya kuvunja ungo, hali ambayo huwafanya wengi wao kuwaingiza wanaume na kulala nao.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel akizungumzia tatizo la mimba kwa wanafunzi, alisema wazazi na jamii wanayo nafasi kubwa ya kusaidia kulimaliza tatizo hilo kwa kujenga maadili kwa watoto. Takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi 170 wa sekondari katika Mkoa wa Geita kwa mwaka 2017 waliacha shule kwa kupata ujauzito huku 90 wa shule za msingi wakishindwa kuendelea na masomo baada ya kupata ujauzito.
Pia, mkoa huo una tatizo kubwa la utoro kwa wanafunzi, takwimu zinaonyesha kati ya wanafunzi 13,139 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2014, ni wanafunzi 7,912 tu ambao ni sawa na asilimia 60 waliomaliza kidato cha nne mwaka 2017.
0 comments:
Post a Comment