Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema wabunge ambao hawafiki kwenye majimbo yao baada ya kuchaguliwa na wananchi kwa kipindi cha miaka mitano, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakata majina yao mwaka 2020.
Alisema wabunge wengi wamekuwa na tabia kutoonekana majimboni na kuacha majimbo yao bila uwakilishi, hivyo kuifanya CCM kuwa na wakati mgumu uchaguzi unapofanyika.
Balozi Seif aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wanachama wa CCM wilayani Kahama wakati akijitambulisha baada ya kuteuliwa na na chama hicho kuwa mlezi wa Mkoa wa Shinyanga kichama, na kusema wabunge wengi wakichaguliwa wanahamishia makazi mjini Dodoma.
Alisema wakifika Dodoma husahau wananchi wao ambao waliwapatia dhamana ya kuwaongoza na kukifanya chama kuwa na wakati mgumu wa kuwanadi watu hao kwa wananchi uchaguzi mwingine unapofika.
“Mbunge ukiona jina lako halijarudi mwaka 2020 ujue umekatwa na Kamati Kuu ya CCM…kutokana na hali hiyo wabunge mnatakiwa kubadilika na kuyatembelea majimbo yenu mara kwa mara na kufanya mikutano na kuzungumza na wananchi wenu, ili kujua changamoto zilizopo na kuzitatua,” alisema Balozi Seif.
Alisema wananchi wamekuwa wakilalamikia kutowaona wabunge wao na kukosa baadhi ya huduma za kijamii na kuongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha wananchi kutokuwa na imani na chama tawala na kuvipatia dhamana vyama vingine kuwaongoza.
Akimuunga mkono kuhusu hoja hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, alisema hata baadhi ya madiwani wanapopata ushindi kwenye kata zao huhamia mijini na kujenga miji mipya.
Alisema chama hakitawavumilia madiwani wa namna hiyo na kitawakata majina na kuweka watu wengine ambao watakuwa na uwezo wa kuwahudumiwa wananchi na kukaa karibu nao muda wote wa miaka mitano.
0 comments:
Post a Comment