Kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyika kuanzia tarehe 29 – 30 Aprili, 2016, kimekamilika Mjini Gisenyi, Rwanda, ambapo wataalam wa sekta mbalimbali wameazimia kuharakisha maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Kikao
hicho cha 14 cha ushirikiano kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa
Tanzania na Rwanda wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
nchini Rwanda mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Wakati
wa ziara hiyo, wakuu hao walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa
makubaliano ya ushirikiano na kuibua maeneo mapya yanayolenga kuinua
shughuli za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Wakati
wa ufunguzi wa kikao hicho cha wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania
Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya
Tanzania aliwakumbusha wajumbe wa pande zote mbili kuendesha mazungumzo
na mjadala kwa kuzingatia maagizo ya viongozi hao na vilevile
kuchangamkia fursa za ushirikiano wa shughuli za kiuchumi za wananchi wa
pande zote mbili baada ya mindombinu ya kikanda kuimarika.
Kwa
upande wake, Balozi Jeanine Kambanda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Nje ya Rwanda na mwenyeji wa kikao hicho, alihimiza wajumbe kujiwekea
malengo yanayotekelezeka na tarehe za ukomo kwenye maeneo yote
watakayokubaliana ili kusukuma utekelezaji na kupata matokeo ya haraka.
Pamoja
na mambo mengine, pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano
katika sekta muhimu kama vile miundombinu ya ushoroba wa kati (central
corridor), kuharakisha ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha
kimataifa (standard gauge), kukuza ushirikiano katika sekta ya anga
hususan baina ya mashirika ya ndege ya Rwandair na ATCL, kuimarisha
ushirikiano katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, kilimo na
ufugaji, utalii, elimu, mawasiliano n.k.
Mkutano
huo pia umekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji (Joint
Implementation Committee) kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu maeneo yote
ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika Kikao hicho cha 14. Kamati hiyo
itakayoongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo
mbili, itakutana kila robo mwaka.
Aidha,
Serikali ya Rwanda imeonesha utayari wake wa kuleta nchini Maafisa na
Watumishi wa Serikali kwa lengo la kupata uzoefu na mafunzo katika vyuo
vya kitaalamu nchini kama vile Chuo cha Diplomasia (CFR), Chuo cha
Taifa cha Utalii na Wanyamapori (Mweka) na Chuo cha Usafirishaji (NIT).
Kwa
upande wa Tanzania, Serikali imedhamiria kuwakutanisha wataalamu wa
mitaala ya elimu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Rwanda kwenye
upande wa kuandaa mitaala ya elimu ya tehama kwenye shule za awali,
msingi na sekondari.
Mkutano
ujao wa kumi na tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya
Tanzania na Rwanda utafanyika mwaka 2018, nchini Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Gisenyi, Rwanda
30 Aprili, 2016
0 comments:
Post a Comment