SERIKALI
imefuta mchakato wa kutangaza ada elekezi tangu katikati ya Mei mwaka
huu, ambapo udhibiti wa ada hizo sasa utafanywa na Kamishna wa Elimu na
Idara ya Ukaguzi.
Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
alisema hayo jana jioni alipokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti ya
wizara hiyo na kuongeza kuwa mchakato huo umefungwa baada ya kujadiliana
na wamiliki na Kamati ya Bunge.
Kwa
mujibu wa Profesa Ndalichako, usimamizi wa utoaji wa michango na ada
holela katika shule hizo utashughulikiwa kwa mujibu wa sera, ambapo
kutatakiwa kuwepo kwa kibali kwanza.
Alisema
kutokana na hatua hiyo ya Serikali, ambayo inalenga kupata muda wa
kutafakari suala hilo na kutafuta namna bora ya udhibiti, sasa
hakutakuwa na ada elekezi ila michango itadhibitiwa.
Awali
katika mjadala, baadhi ya wabunge walipinga mchakato huo na kutaka
Serikali kujikita katika kuboresha shule zake na kuachana na utoaji wa
ada elekezi.
Akizungumza
katika mjadala huo, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisema
hakuna sababu ya kuwa na ada elekezi kwa shule binafsi.
Lugola
alisema kama Serikali ikitaka shule binafsi zife, ni kuwalipa vizuri
walimu wake, kuwajengea nyumba zao, kuwa na madarasa na kuweka chakula
na hayo yakikamilika, hakuna mtu binafsi atakayepandisha ada.
Kwa mujibu wa Lugola, kama hayo hayatafanyika, kila mtu ana uamuzi wa kumpeleka mtoto katika shule anayotaka hata Ulaya.
“Kuna
tatizo gani na hizi shule za binafsi? Kwanza wamerundikiwa kodi nyingi
mara kupaka rangi magari na mengineyo, sasa watarudishaje hizo fedha?
Ndiyo maana wanatoza ada kubwa,” alitetea.
Naye
Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Hassan (Chadema), alielezea kushangaa ni
kwa jinsi gani ada elekezi itawekwa, wakati hakuna viwango vya utoaji
elimu kwa watoto.
Mbunge
wa Maswa, Mashimba Ndaki (CCM), alisema suala hilo la ada elekezi
watakaonufaika ni watu wenye fedha kwani ndiyo wanaowapeleka watoto
katika shule binafsi na kusahau kuboresha shule za Serikali ambazo ni
kwa watu wenye vipato vya kawaida.
Ndaki
alisema iwapo shule za Serikali zingekuwa bora, zingechukua wanafunzi
wote na zile za binafsi zingekosa wateja kwa gharama zao hizo kubwa,
hivyo hakuna sababu ya kuwawekea ada elekezi.
“Shule
binafsi wanapata wateja kutokana na miundombinu mibovu, matatizo ya
walimu yanayotokana na kutotendewa haki katika shule za Serikali tofauti
na shule binafsi ambazo wanawathamini walimu na kufanya watoe elimu
bora,” alisisitiza.
Alitaka
waziri, badala ya ada elekezi angekuja na mkakati madhubuti wa
kuboresha shule za Serikali kwa kuwapa mahitaji yao walimu, kununua
vitabu mashuleni na kuboresha miundombinu na shule hizo na hilo
lingesababisha wapunguze wenyewe ada zao.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Ester Mahawe (CCM) alisema Sheria ya Elimu ya 1978,
inasema elimu siyo biashara bali huduma, lakini sasa wanaotoa elimu hiyo
binafsi wanaonekana kama wao ni maadui.
Alisema
shule binafsi, zinasaidia kusomesha Watanzania lakini bila kuthaminiwa
wakati nchi nyingine watu binafsi wanasaidiwa kuwalipa mishahara, hapa
nchini wanawapiga chini licha ya kuwa wanasaidia kusomesha hata watoto
yatima, ili kuondoa watoto wa mitaani huku akieleza yeye katika shule
yake anasomesha watoto 67.
Mahawe
alisema shule binafsi wanalipa kodi zaidi ya 10, licha ya kuwa wameokoa
kupeleka watoto kusomeshwa katika nchi za Kenya na Uganda huku akiomba
wizara kuwapatia dawati wizarani ili wawape ushauri hususan katika
mitaala.
0 comments:
Post a Comment