Meneja kanda ya ziwa mr Moses.Mbambe |
Na.
Mwandishi Wetu
Wakati
serikali ikiendelea kukabiliana na changamoto ya uhaba wa bidhaa ya sukari na
ongezeko la bei ya bidhaa hiyo, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Ofisi ya
Kanda ya Ziwa imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya matumizi ya sukari ya Kijiko
Kimoja (KK).
Sukari
ya Kijiko Kimoja inatengenezwa na kiwanda cha 21st Century Food
& Packaging Ltd kilichoko Dar es Salaam. Sukari hii ni nyeupe na imetengenezwa
kwa kutumia miwa kwa silimia 99.5 na asilimia 0.5 ya vikolezo vingine nyongeza vya
utamu.
Akiongea
na wajasiliamali wa jijini Mwanza katika Semina ya Elimu kwa Umma iliyofanyika
katika Shule ya Sekondari ya Mwanza, Mkaguzi Mwandamizi wa Chakula wa TFDA
Kanda ya Ziwa Julius Panga alisema kuwa kumekuwa na taarifa juu ya baadhi ya watumiaji
wakikiuka maelekezo ya matumizi na wafanyabiashara kuuza sukari hiyo kinyume na
taratabu.
Panga
alisema kuwa sukari ya Kijiko Kimoja ni tamu kuliko sukari nyingine kwa kuwa
kijiko kimoja ni sawa na vijiko viwili na kuwa kutokana na hali hiyo wazalishaji
wameweka taarifa juu ya kifungashio ambazo zinatoa maelekezo juu ya namna ya
kutumia bidhaa hiyo.
“Sukari
hii ina kiwanngo cha juu cha utamu tofauti na sukari nyingine ambazo zinatumika
nchini. Hali ambayo imepelekea wagonjwa wa kisukari, wanawake wajawazito na
watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kutoruhusiwa kuitumia” alisema
Panga.
Panga
aliongeza kuwa kutokana na upungu wa bidhaa ya sukari nchini baadhi ya wafanyabiashara
wamekuwa wakiiondoa sukari hii katika vifungashio vyake na kuuzwa rejareja hali
ambayo ni hatari kwa mtumiaji kwani anakuwa hapati taarifa zilizoko katika
kifungashio. “Watengenezaji wa sukari hii wameifungasha katika vifungashio vya
kilo moja na nusu kilo. Juu ya vifungashio kuna taarifa muhimu ambazo mteja
anapaswa kuzisoma kabla hujatumia. Wauzaji wanapotoa sukari katika vifungashio
vyake wanamnyima mteja haki ya kupata taarifa na kufanya uamuzi. Vitendo hivi
vimekuwa vikiripotiwa katika maeneo mbali mbali ya kanda ya ziwa”.
Pia
Panga alisema kuwa wauzaji wa chai katika baadhi ya migahawa wamekuwa wakitumia
sukari ya kijiko kimoja hali ambayo ni
hatari kwa afya ya wateja kutoka katika makundi yaliyoanishwa juu ya
kifungashio “ Ndani ya migahawa wanaingia watu wote hata wale ambao
hawaruhusiwi kutumia sukari hii. Si vizuri kutumia sukari hii katika maeneo
haya. Tunashauri wafanyabiashara wa migahawa kutumia sukari nyingine ambayo
inaruhusiwa kwa makundi yote” alisema.
Maria
Paskari ni mkazi wa Kirumba jijini Mwanza, yeye anakili kutumia sukari ambayo
ilikuwa tamu kuliko sukari nyingine ambayo amekuwa akitumia. “ Nilimuagiza
mtoto kwenda kununua sukari robo dukani. Alileta sukari nyeupe ambayo ilikuwa
ni tamu tofauti na ambayo nilikuwa nimeizoea” alisema.
Maria
anasema kuwa hakuwahi kusoma maelezo yaliyokuwa katika kifungashio.
“Sijawahi
kuona sukari hii ikiwa katika vifungashio vyake. Lakini na mshukuru Mungu mimi
sio mjamzito na watoto hawakuitumia. Niliitumia mwenye kwa kuweka kwenye uji
ambao watoto hawakuunywa” alisema
Kwa
upande wake muuzaji wa duka la ‘Mke Mwema’ ililiko Igombe nje kidogo ya jiji la
Mwanza Bw. Justin Ntahorija alisema kuwa hajawahi kuuza sukari hiyo lakini baadhi
ya wateja wamekuwa wakiwatuma watoto sukari wakiwapa maelekezo kuwa wasinunue
sukari nyeupe. “Juzi alikuja mtoto akitaka sukari lakini akanieleza kuwa
ameagizwa asinunue sukari kama iliyokuwa kwenye kifungashio alichokuwa
amekishika. Nilivyoangalia kifungashio nikakuta ni kile cha sukari ya kijiko
kimoja” alisema.
Bw
Ntahorija aliongeza kuwa katika maeneo ya Igombe kuna taarifa nyingi za
kukanganya kuhusu sukari. “Zipo taarifa zinazagaa kuwa sukari nyeupe si nzuri
kwa matumizi ya binadamu na atakayekutwa nayo anakamatwa.”alisema.
Hata
hivyo Panga alisema kuwa Sukari ya Kijiko Kimoja imesajiliwa na Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA) kama zilivyo bidhaa nyingine za sukari na hivyo kufaa
kwa matumizi. “Wananchi hawapaswi kuogopa kununua na kutumia sukari ya Kijiko Kimoja
na sukari nyingine nyeupe. Wanachopaswa kufanya ni kufuata maelekezo yaliyoko
juu ya kifungashio. Pia wafanyabiashara wanao wajibu wa kuwalinda wateja wao
kwa kuhakikisha wanawapatia bidhaa zinazofaa”alisema Panga huku akitoa rai kwa
wananchi kujenga tabia ya kusoma taarifa juu ya vifungashio.
"God who created you without you, will not save you without you" St. Augustine of Hippo (354-430)
0 comments:
Post a Comment