Marehemu Yohana Albogasti.
Issa Mnally na Richard Bukos, UWAZI
DAR ES SALAAM: Yohana Albogasti,
21, (pichani)mkazi wa Majohe Viwege Kwampemba jijini Dar ameuawa kwa
kupigwa risasi chumbani akiwa mtupu, Uwazi limeipata.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, tukio hilo lilijiri usiku wa Mei 13, mwaka huu huko Majohe ambapo marehemu alikuwa ametoka kuoga.
“Mimi nilisikia mlio wa risasi mara moja
tu. Nilikuwa na wenzangu, wote tulikaa kimya kila mmoja akihofia
kusogelea eneo hilo kwani hatukujua kilichokuwa kikiendelea,” alisema
shuhuda mmoja.
Akaendelea: “Kwa kuwa jirani na eneo
hilo kuna jumba la kifahari linalomilikiwa na mfanyakazi wa Tanesco
(Shirika la Umeme Tanzania) tulijua majambazi wamevamia kwake.
“Baada ya dakika kadhaa, watu tulianza
kwenda eneo la tukio. Ndipo tulipoukuta mwili wa marehemu ukiwa chini
hatua chache kutoka nyumba aliyokuwa akiishi.
“Alipigwa risasi chini ya titi la kushoto. Inaonekana alitoka ndani ili kujiokoa lakini alianguka sehemu hiyo akiwa mtupu.”
Jirani
mwingine aliyedai kushuhudia tukio hilo alisema akiwa eneo hilo
alisikia sauti ya mwanamke ikipiga kelele kuomba msaada kisha alimuona
mwanaume mmoja akitoweka baada ya mlio wa risasi.
Uwazi pia lilizungumza na mume wa marehemu, Pazi Hamis (23) ambaye alisema:
“Kwa kweli hata mimi nashangaa sana,
sijui hawa wauaji walikuwa na kisa gani na mke wangu kwani marehemu
hajawahi kuniambia jambo lolote ambalo ningelihusisha na tukio hilo.
“Siku
ya tukio, saa mbili usiku nikiwa kwenye mihangaiko nilipigiwa simu na
jirani na kupewa taarifa. Sikuwa na jinsi, niliwahi eneo la tukio.
“Nilimkuta mke wangu amelala kifudifudi
akitoka damu nyingi chini ya ziwa. Polisi nao walifika, wakauchukua
mwili hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuuhifadhi.
“Kwangu kifo hiki ni pigo kubwa, kaniachia mtoto Halima ana miaka miwili. Yeye pia alikuwa na ujauzito wa miezi sita.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Ilala, SACP Lucas Mkondya alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kusema mtuhumiwa mmoja ameshakamatwa, wengine wanasakwa.
“Mtuhumiwa huyo jina tunalihifadhi kwa ajili ya uchunguzi, mwingine ametoroka.
“Tukio
lenyewe linaonekana kuwa na utata kwa kuwa marehemu alikuwa akiishi
maisha ya hali ya chini, yaani hakuwa na pesa za kuweza kuvamiwa.
“Yawezekana kuna visasi! Hilo ndilo
jambo tunaloendelea kulifanyia uchunguzi wakati tukiendelea kumsaka
mtuhumiwa aliyetoroka,” alisema Mkondya.
Marehemu amezikwa Jumanne iliyopita kwenye Kijiji cha Kisaki Kata ya Singisa, Matombo mkoani Morogoro.
0 comments:
Post a Comment