Wakili Hashim Spunda.
*Azungumzia mbinu ya kupunguza bei ya sukari, asema watu wana njaa!
MMOJA wa wagombea Urais na Mwenyekiti wa
Taifa wa Chama cha Umma (Chauma), Wakili Hashim Spunda Rungwe amefanya
mahojiano maalum na wahariri wetu ili kutoa tathmini yake ya utawala wa
miezi sita wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli
tangu ashike madaraka ya kuongoza nchi. Wakili Rungwe ameshauri mambo
mazito ya nini cha kufanya ili nchi iweze kusonga mbele kimaendeleo.
Hata hivyo, ametoa maoni juu ya mjadala wa Bunge kutooneshwa laivu na
sakata la sukari, fuatana nasi katika makala haya ujue kile
alichokisema:
Tupe maoni yako kuhusu utawala
wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye amefikisha miezi sita akiwa
madarakani, je, anakwenda vizuri?
Rungwe: Miezi sita ya
Serikali ya Awamu ya Tano sijasikia mpango wowote wa kuondoa njaa kwa
wananchi. Lazima rais ajue kwamba watu wana njaa na zifanyike juhudi
kuhakikisha kipato kwa mwananchi mmojammoja kinaongezeka badala ya
kupungua na bei ya vyakula inapungua. Maana yake ni kwamba vyakula
vipungue bei badala ya kuongezeka. Kwa mfano, sukari ilikuwa Sh. 1,800
sasa ni zaidi ya Sh. 3,000 kwa kilo. Hili ni tatizo. Nitoe ushauri wa
bure kwa Rais Magufuli, asihubiri ubaya wa baadhi ya watu hadharani kwa
sababu kunaweza kuwafanya wawekezaji kuogopa kuja kuwekeza nchini.
Yapo mambo ambayo anapaswa kuongea na
watendaji wake tu na mambo yakaenda bila kuwafanya watu wa nje kujua
kuwa Tanzania ni nchi ambayo unaweza kunyang’anywa mali yako bila
kufuata utaratibu wa kisheria. Huu ni ushauri tu, nimeutoa kwa faida ya
nchi.
Nini maoni yako kuhusu Bunge kutorushwa laivu?
Rungwe: Kwanza ieleweke
kuwa kuzuia Bunge kuoneshwa laivu ni ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya
habari lakini pia ni kuwanyima wananchi kuwaona wabunge wao
wanavyojadiliana juu ya maisha yao. Tusifuatishe nchi nyingine, kama
sisi tuliamua kufanya hivyo na wananchi wakaona inafaa, kuna ubaya gani
nchi za nje zikituiga sisi? Kwa maneno mengine kutoonesha bunge laivu
tunaweza kusema huu ni utemi wa wazi. Hakuna sababu yoyote ya msingi ya
kuwanyima wananchi haki yao ya kumuona mbunge wao akitoa hoja zao kwani
ndivyo katiba ya nchi yetu inavyosema tofauti na katiba nyingine.
Katika miezi sita hii tumeshuhudia watumishi wa sekta za umma wakitumbuliwa majibu, je, una maoni gani kuhusiana na zoezi hilo?
Rungwe: Mimi kama
wakili nashauri viongozi wa serikali wa ngazi zote wasifukuze
wafanyakazi hovyohovyo bila kuwasikiliza. Kufanya hivyo ni ukiukaji wa
sheria, kwani katika sheria tunaambiwa usihukumu kwa kusikiliza hoja za
upande mmoja. Usimhukumu unayemuona muovu kwa kufanya uovu. Ushauri
wangu ni kwamba wanaosimamishwa wote, wasikilizwe, huo ndiyo utawala wa
kisheria.
Ndani ya miezi sita kuna
changamoto nyingi katika serikali, kuhusu sekta ya elimu kuna uhaba wa
madarasa na madawati, unasemaje kuhusu hilo?
Rungwe: Ili kumaliza
changamoto hiyo niseme tu kwamba serikali iache matumizi makubwa kama
vile viongozi kujinunulia magari ya kifahari, fenicha mpya, kujilipa
posho nono na kuwasaidia watu kukwepa kodi kama ilivyokuwa miaka ya
nyuma, badala yake wajenge nchi kwa kufanya kazi kwa bidiii na kwa
kusaidiana na wananchi wenye nia njema kuchangia maendeleo, matatizo
hayo yatakwisha.
Hivi sasa kuna tatizo kubwa la mfumuko wa bei ya vyakula, unadhani serikali ifanye nini kuondoa kabisa tatizo hilo?
Rungwe: Serikali
isitafute mchawi, mchawi ni yenyewe kutokana na mfumo uliokuwepo tangu
zamani. Marais waliopita ni watu wa timu yake Rais Magufuli na
nisiwatetee, hao wamesababisha haya. Tulikuwa na mashirika ya umma mengi
kama vile Bhesco, RTC, Hosco, NBC na kadhalika lakini mengi yamekufa
kutokana na kuwekwa watu kuongoza wasio na uzoefu.
Mfumuko wa bei upo, kwa mfano, hili la
sukari ni tatizo kubwa kwa sababu hivi sasa kikombe cha chai ya rangi
kwa mama ntilie ni shilingi 500 badala ya shilingi 200. Hii utaona kuwa
haijamsaidia mlalahoi, watu wana njaa, serikali itafute mbinu ya kuondoa
adha kama hii. Bei ya Dizel, ipungue kila kitu kitapungua bei kwa
sababu vyakula vinasafirishwa kutoka shambani kwa gharama kubwa.
Sukari ya nje imezuiliwa kuingia nchini nini ushauri wako?
Rungwe: Mimi ningekuwa
mshauri wa rais, ningemshauri asizuie kuagizwa sukari kutoka nje badala
yake ningeshauri waitoze ushuru mkubwa na hii inayozalishwa nchini
ikaondolewa ushuru. Kwani kuna hasara gani kuondoa ushuru kwa commodity
(bidhaa) moja? Ni wazi watu wangekimbilia sukari ya bei nafuu.
0 comments:
Post a Comment