Mwandishi Makongoro Oging’ enzi za uhai wake.
“Makongoro Oging’ amefariki
dunia,” yalikuwa ni maneno yaliyopenya masikioni mwangu kutoka kwa Oscar
Ndauka, Mhariri Kiongozi wa Global Puplishers alipofika nyumbani kwangu
Jumamosi usiku wa Mei 21, mwaka huu akiwa na Sifael Paul, Mhariri wa
Gazeti la Ijumaa Wikienda.
Nilipigwa na butwaa kusikia
habari hiyo ambayo kama ningekuwa na matatizo ya kiafya ningeweza kupata
presha, huku mke wangu akishikwa na mshangao na akihoji kama vile
hakusikia: “Makongoro kafariki duni?”
Tar
14.8.2015 Makongoro akimuhoji mke wa aliyekuwa askari wa gereza la
Dondwe Pwani ambaye aliuawa katika uvamizi wa kituo cha Stakishari,
Picha na Richard Bukos.
Nilimuona akifuta machozi kwa khanga,
kisha nami nikachukua kitambaa na kufuta machozi. Tulizungumza mengi
hadi saa nane usiku kupanga tufanyeje kesho kukicha baada ya kuzungumza
na mke wa Makongoro usiku huo huo na kututhibitishia habari hiyo.
Jina la Makongoro Oging’ siyo geni kwa
watu wanaofuatilia habari hasa wasomaji wa magazeti ya Global Publishers
hususan Gazeti la Uwazi.
Ni juzi tu aliniletea fomu zake za
kutaka press card na alipoijaza ikaonesha kuwa yumo ndani ya tasnia ya
habari kwa miaka 21 sasa, hivyo kutosha kusema kwamba ni mkongwe katika
fani hii.
Makongoro alikuwa mahiri wa kuandika
habari za uchunguzi kwani mwaka 2004 alipewa tuzo ya mwandishi bora wa
habari hizo, iliyotolewa na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal
Tanzania kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.
Miongoni mwa watu waliotunukiwa tuzo
siku hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa pamoja na waandishi
wa habari wengine ambao majina yao siwezi kuyakumbukwa kwa sasa.
Alistahili kwa sababu Makongoro
alipokuwa kazini hakuwa na mchezo. Alikuwa akifuatilia habari za
uchunguzi kwa kina. Nakumbuka siku moja aliandika habari moja ya
udhalilishaji uliofanywa na vijana fulani baada ya kumteka msichana
mmoja na kumpiga sana kisha kumvua nguo.
Sakata hilo lilifika jeshi la polisi
wakati huo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Kamishna Mstaafu Alfred
Tibaigana akiwa madarakani alinipigia simu na kunitaka niende na
Makongoro ofisini kwake ‘ sentro’.
Tulipofika tu akatuona tupo kwenye
korido akasema kwa sauti, “Kamanda Zombe ( Abdallah), watu wa Uwazi
wamefika, Makongoro uliyekuwa ukimtafuta huyu hapa, kaja na bosi wake.”
Zombe aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa
polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam wakati ule, alikuwa kwenye
chumba kimoja na aliposikia sauti ya bosi wake alitoka na kutulaki huku
akitukaribisha.
“Karibuni sana.”
“Ahsante.”
“Tumekuwa tukifuatilia gazeti lenu la
Uwazi na habari ya wiki hii ipo mezani kwangu naomba mtusaidie mawili
matatu,” alisema Zombe.
Baadaye alitukabidhi kwa askari mmoja wa upelelezi ambaye namkumbuka kwa jina moja tu la Judi ili tufanye naye mahojiano.
Judi alituchukua hadi ofisini kwake na
kuanza kunihoji mimi kwa dakika chache kama mhariri wa habari ile na
baadaye akaanza kumhoji Makongoro ambaye alichukua muda mrefu kutokana
na mambo mengi ambayo alikuwa anayajua kuhusiana na habari ile.
Baada ya mahojiano yale Kamanda
Tibaigana alituita ofisini kwake na kusifia umahiri wa Makongoro katika
kuandika habari za uchunguzi na akasema huwa zinamsaidia sana katika
uchunguzi wa tuhuma mbalimbali ambazo zinawafikia.
Tangu siku hiyo Makongoro Oging akawa
rafiki wa Tibaigana na Zombe pamoja na askari wengine wengi pamoja na
mawakili akiwemo Mabere Marando hali iliyofanya awe mahiri wa kuandika
habari zinazohusu watuhumiwa mbalimbali.
Ilikuwa siyo rahisi kwa Makongoro kwenda
kwenye kituo fulani cha polisi na kukosa ushirikiano anapofuatilia
jambo kutokana na uhusiano mzuri alioujenga na askari hao hata wale wa
Magereza na Kikosi cha Zima Moto.
Kwa upande wa wagonjwa katika hospitali
mbalimbali, Makongoro alikuwa akiwaandika sana na kuwaombea misaada kwa
wasomaji wa Gazeti la Uwazi na alifanikiwa kuwawezesha baadhi yao
kupelekwa nje ya nchi kutibiwa kwa kuchangiwa na wasomaji.
Wengine walipelekwa India, wengine
hospitali za humu ndani na kubadili maisha yao baada ya kutibiwa na
kupona kutokana na kalamu yake aliyoitumia kwa manufaa ya jamii.
Wapo watu ambao walikuwa na maisha duni
lakini Makongoro kwa kutumia kalamu yake aliandika habari zao na baadhi
yao kufanikiwa kujengewa nyumba za kisasa.
Kwa upande wa wanafunzi, Makongoro
hakuwaacha nyuma, nao alikuwa akiwafuata na kuandika matatizo yao. Wapo
waliokuwa wakikwama kimasomo kutokana na wazazi wao au walezi wao
kushindwa kuwalipia ada, mwandishi huyu aliandika habari zao na baadhi
yao wakafadhiliwa na kusoma hadi chuo kikuu.
Makongoro hakuwa mchoyo wa fani yake,
nimemshuhudia zaidi ya miaka 15 akiwafundisha waandishi chipukizi habari
za uchunguzi na kuwa wa kutumainiwa katika chumba cha habari.
Alikuwa akipenda kuwafundisha uandishi
wa uchunguzi waandishi chipukizi kivitendo kwani baadhi yao alikuwa
akiongozana nao kwenye matukio na kuwafundisha kivitendo jinsi ya
kufuatilia habari za uchunguzi alizokuwa akiziandika enzi za uhai wake.
Kazi yake ilimfanya ajulikane sehemu
nyingi, kama vile ndani ya majeshi yetu yote, katika hospitali kubwa,
mitaani na hata kwenye mashirika na taasisi za umma na zile binafsi.
Alikuwa jasiri kwa kufuatilia jambo bila
woga na ndiyo maana mpaka anaaga dunia Jumamosi saa moja jioni
hatukuwahi kuwa na kesi kwenye gazeti iliyosababishwa naye.
Makongoro ameacha mjane na watoto watatu. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
0 comments:
Post a Comment